Kikao cha kamati ya halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi
(CCM), wilaya ya Geita kimemtimua katibu msaidizi wa wilaya hiyo Patrick Kusaga
kwa kile kinachodaiwa kutafuna fedha za mapango ya nyumba ya chama hicho zaidi ya sh. Milioni 6.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mkutano
wa chama hicho katibu mwenezi wa wilaya Jonathan Masele, alisema wamefikia
maamuzi hayo ya kumuondoa na kufunga ofisi yake kwa ubadhilifu mkubwa wa fedha
na dharau kwa viongozi wenzake.
Masele alisema kamati ya siasa ya wilaya
imekuwa ikimwita mara kwa mara ili
kuzungumzia tuhuma zake lakini amekuwa akiwatolea majibu ya kejeli, jambo
ambalo limepelekea kumuondoa.
“Tumefikia maamuzi haya kutokana na Katibu huyu msaidizi
kujiona yeye ni zaidi ya wenzake na kujipa madaraka makubwa na amehusika na upotevu
wa sh. Milioni 6 za kodi kutokana na hayo, kamati ya siasa ya wilaya imemwita mara kadhaa
lakini ameshindwa kutii wito na amekuwa akitutolea lugha za kejeli kuwa sisi
hatuwezi kumfanya chochote kwa kuwa anawakubwa ambao wanamlinda”.
“Kamati ya siasa ya wilaya hatumtaki labda Mkoa au makao
makuu wampeleke wanakojua wao lakini hapa hatumhitaji, anasababisha chama
kiyumbe na anaweza kusababisha chama tulikose hili jimbo la Geita, tumeamua
kufunga na ofisi yake hapa tunasubiri kuletewa mtu mwingine huyu hafai kabisa
kuwa hata balozi kwa ufisadi wake.. kadi za ccm tunaziuza sh. 300 lakini yeye
anaziuza sh 540 kinyume na utaratibu,.”alisema Masele.
Waandishi wa habari walilazimika kumtafuta Patrick Kusaga ili kujua tuhuma hizi zinazomkabiri ni za
kweli ama la, alisema yeye hajui lolote juu ya hilo na alikuwa Butiama kwenye
msiba wa mtoto wa Mwl. Nyerere.
“Hizo tuhuma mimi sizijui na sijaitwa na tunapoongea nipo
Mwanza natoka Butiama kwenye msiba wa mtoto wa mwl. Nyerere’’alisema Kusaga.
Hata hivyo mara baada ya waandishi wa habari kumaliza kuongea
na Kusaga, Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Mkoa wa Geita Joseph Msukuma
alipiga simu kwa mmoja wa waandishi akimtaka asiandike chochote juu ya habari
hiyo.
Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita
Social Plugin