Mtoto mmoja Reuben
Daud(3) mkazi wa Nyihogo wilayani Kahama mkoani Shinyanga amefariki
dunia leo baada ya kutumbukia kwenye karo la choo ambapo mazingira ya
tukio hilo hayakufahamika.
Kwa mujibu wa mashuhuda
wa tukio hilo wamesema mnamo saa 3 ya asubuhi kulizagaa taarifa ya
kupotea kwa mtoto katika eneo hilo na ndipo jitihada za kumtafuta
zikafanyika na kumkuta akielea kwenye karo la choo nyumba ya jirani
amefariki.
Mmoja wa mashuhuda hao
Khalfan Mohamed ameelezea tukio hilo kuwa alisikia taarifa za kupotea
kwa mtoto ambapo baadae taarifa za kupatikana kwa mtoto huyo akiwa
ameelea kwenye karo, hivyo taratibu za kuuopoa mwili zikafanyika.
Kwa upande wa baba mzazi
wa mtoto huyo Daud Reuben ameelezea tukio hilo kuwa mtoto aliondoka
kwenda kununua kitafunwa kwa ajili ya chai lakini hakurudi ndipo
walipowashirikisha majirani kumtafuta ambapo walimuona kwenye karo hilo
akiwa amefariki.
Naye mtendaji wa mtaa
huo Simon Mabumba amesema uzembe wa kuacha makaro wazi ndiyo chanzo cha
matukio kama hayo kuendelea kujitokeza hivyo wananchi wanapotaka kujenga
wanapaswa kuzingatia usalama wa jamii na si kuangalia shughuli zao tu.
Jeshi la Polisi wilayani
Kahama lilifika katika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu na
kisha kuupeleka chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya
ya Kahama kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Social Plugin