TAARIFA YA KUKAMILIKA KWA KAZI YA TUME YA UCHUNGUZI WA MALALAMIKO YALIYOTOKANA NA UTEKELEZAJI WA OPERESHENI TOKOMEZA
___________________________________________
1.0 Utangulizi:
1.1
Tarehe 01/05/2014, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete aliunda Tume ya Uchunguzi kuhusu malalamiko
yaliyotokana na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Aliteua Makamishna
watatu ambao ni Mhe.
Balozi
Jaji (Mst) Hamisi Amiri Msumi (Mwenyekiti wa Tume), Mhe. Jaji (Mst)
Stephen Ernest Ntashima Ihema (Kamishna), Mhe. Jaji (Mst) Vincent
Kitubio Damian Lyimo (Kamishna) na Ndugu Frederick Kapela Manyanda
(Katibu wa Tume).
1.2
Operesheni Tokomeza ilikuwa Operesheni iliyobuniwa na Wizara ya
Maliasili na Utalii kwa lengo jema na muhimu la kupambana na ujangili
unaotishia urithi wetu wa wanyama pori, hususani tembo, faru, nyati,
twiga, pundamilia n.k.
2.0 Hadidu Rejea kwa Tume
2.1Kuchunguza namna Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa;
2.2.Kuchunguza iwapo maafisa waliotekeleza Operesheni Tokomeza walizingatia sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa;
2.3.Kuchunguza iwapo maafisa waliotekeleza Operesheni Tokomeza walivunja sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea walizopewa;
2.4.Kuchunguza
iwapo kuna watu waliokiuka sheria yoyote wakati wa utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza na iwapo hatua zilizochukuliwa na maafisa wa
Operesheni Tokomeza dhidi ya wakosaji hao na mali zao zilikuwa sahihi;
2.5.Kupendekeza
hatua zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya maaafisa wa Operesheni
Tokomeza waliokiuka sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea za
Operesheni Tokomeza; na
2.6.Kupendekeza
mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika kupanga na kutekeleza Operesheni
nyingine kama hii ili kuzuia na kuepuka malalamiko mengine kama
yaliyotokea kwenye Operesheni Tokomeza.
3.0 Kukamilika kwa kazi ya Tume
3.1
Tume imekamilisha kazi yake na kukabidhi taarifa kwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 10
Aprili, 2015. Kwa maagizo ya Rais tumeisoma na kuichambua taarifa hiyo
vya kutosha.
Kwa
hakika Tume imefanya kazi kubwa sana, na nzuri sana ya uchunguzi na
uandishi wa taarifa. Kazi imefanywa kwa weledi na umakini wa hali ya juu
na kwa lengo dhahiri la kutenda haki. Katika siku 265, Tume ilitembelea
wilaya 38 katika mikoa 20 na kuhoji jumla ya mashahidi 259.
Mikoa
iliyohusika ni Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya, Kagera, Geita, Shinyanga,
Simiyu, Mara, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Pwani, Tabora,
Singida, Manyara, Arusha na Tanga.
3.2
Tume imejitahidi kuwahoji wote waliokuwa na malalamiko, kuwahoji
mashuhuda, kuwahoji watuhumiwa, na kukusanya ushahidi wa aina mbalimbali
ili ama kuthibitisha makosa pale yalipofanyika na kupendekeza hatua za
kuchukua, au kujiridhisha kuwa tuhuma na malalamiko hayakuwa ya msingi.
Kazi hiyo imefanywa vizuri na kurahisisha kazi ya Serikali ya kuchukua hatua zinazostahili.
4.0 Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa
4.1
Tume ilibaini kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja cha utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza iliyoanza tarehe 4 Oktoba, 2013, mafanikio mengi
yalipatikana, ikiwemo:
4.1.1
Watuhumiwa 1,030 wa makosa mbalimbali yanayohusu ujangili na uvunaji
haramu wa misitu walikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria;
4.1.2
Kukamatwa kwa meno ya 211 yenye uzito wa kilo 522, meno ya ngiri 11,
mikia ya wanyama mbalimbali 36, ngozi za wanyama mbalimbali 21, pembe za
swala 46, mitego ya wanyama 134, ng’ombe 7,621 waliokuwa wanachungwa
ndani ya hifadhi na misitu, baiskeli 58, pikipiki 8 na magari 9;
4.1.3
Katika kipindi cha Operesheni kulikamatwa jumla ya bunduki za kijeshi
18, bunduki za kiraia 1,579, risasi 1,964, mbao vipande 27,913, mkaa
magunia 1,242, magogo 858 na misumeno 60.
4.1.4
Operesheni ilifanikiwa kupunguza kasi ya mauaji ya tembo kutoka tembo
wawili kwa siku hadi tembo wawili kwa mwezi wakati wa Operesheni;
4.2 Operesheni
ilisitishwa rasmi tarehe 01/11/2013 ili kupisha uchunguzi wa malalamiko
yaliyojitokeza. Baada tu ya kusitishwa kwa Operesheni wafugaji wengi
wamerudisha mifugo yao katika maeneo ya hifadhi yaani Mapori ya Akiba,
Hifadhi za Taifa, Hifadhi za Misitu na Maeneo Oevu na ujangili ukaanza
kurejea.
Aidha watuhumiwa waliokuwa wametoroka kukimbia Operesheni wameanza kurejea kwenye makazi yao.
5.0 Vitendo vya Ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu Rejea
5.1
Tume imebaini kuwa katika utekelezaji wa Operesheni kulikuwa na matukio
ya ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Hadidu Rejea. Ukiukwaji huu
umesababisha madhara kwa wananchi mbalimbali ikiwemo vifo, madhara ya
mwili na kadhalika.
5.2
Tume ilichunguza matukio 15 ya vifo, na kuridhika kuwa vifo tisa (9)
kati ya hivyo vilisababishwa na mateso ambapo watendaji kwenye
Operesheni walitumia nguvu kubwa kupita kiasi dhidi ya watuhumiwa wakati
wa ukamataji au kuhoji.
Kabla
ya vifo watu hao walikuwa chini ya ulinzi wa askari wa Operesheni na
kuna ushahidi wa kitabibu (medical reports), ushahidi wa kimazingira na
ushahidi wa kuona, unaohusisha vifo vya marehemu hao na mateso kutoka
kwa askari wa Operesheni.
Tume haikupata ushahidi wa kuhusisha vifo sita (6) vilivyobaki moja kwa moja na Operesheni Tokomeza.
5.3
Tume ilichunguza madai ya mateso yaliyosababisha madhara kwenye miili
ya wahusika. Walalamikaji walieleza Tume kwamba waliteswa ili waoneshe
silaha au nyara zilipofichwa au wakiri kujihusisha na ujangili au
ujambazi na wataje washirika wao wa mtandao wa ujangili.
Kulikuwa
pia na malalamiko ya udhalilishwaji. Malalamiko hayo yalitoka kwenye
wilaya ishirini na mbili (22) za mikoa mbalimbali.
Yapo
matukio ambayo walalamikaji waliweza kuleta mbele ya Tume uthibitisho
wa kuteswa, na walionesha makovu na kutoa vyeti vya matibabu na PF 3
walizopewa baada ya kuumia.
5.4
Tume imebaini kuwepo matendo mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria, kanuni,
taratibu na hadidu rejea uliofanywa na baadhi ya askari wa Operesheni
na maafisa wengine walioshiriki katika utekelezaji wake, ikiwemo matukio
yanayoashiria rushwa na udanganyifu mbalimbali.
5.5
Tume ilishughulikia pia tuhuma za wizi, upotevu na uporaji wa mali.
Walalamikaji wa kundi hili walieleza Tume kuwa wakati wa utekelezaji wa
Operesheni, waliibiwa au kupoteza fedha na mali zao wakati na baada ya
kukamatwa au kupekuliwa na askari wa Operesheni.
Tume
ilichunguza jumla ya matukio ishirini na tatu (23) ya aina hiyo na
kubaini kuwa malalamiko mengi yalitokana na askari wa Operesheni
kutofuata sheria, kanuni na taratibu za ukamataji, kuhoji na upekuzi
maungoni mwa watuhumiwa na kwenye nyumba zao.
Kasoro
zilizoonekana ni pamoja na kutoshirikisha viongozi au watu huru katika
upekuzi na kutojazwa hati za upekuzi mara baada ya upekuzi. Kasoro
nyingine ni askari wengi kuingia kwenye nyumba kwa wakati mmoja.
Aidha,
Tume imebaini walalamikaji wengine waliongeza chumvi katika ushahidi
wao kuhusu idadi ya mali na fedha zilizopotea au kuibiwa na hivyo
ushahidi wao kutoaminika au kuthibitika.
5.6
Tume ilichunguza malalamiko ya kubakwa wakati wa utekelezaji wa
Operesheni. Matukio yaliyochunguzwa na Tume yalikuwa katika Kijiji cha
Iputi, Wilaya ya Ulanga, Mkoa wa Morogoro na Kijiji cha Mwantimba Wilaya
ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu na Wilayani Sikonge.
Hata
hivyo wote waliodai kubakwa hawakujitokeza mbele ya Tume kutoa ushahidi
wao, hivyo Tume haikuweza kuchunguza malalamiko yao.
Alijitokeza
mlalamikaji mmoja Wilayani Ulanga, Morogoro, lakini Tume haikuridhika
na maelezo yake, ambayo hayakutosheleza kubainisha kosa kwenye
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza.
5.7
Tume ilibaini kuwa wapo watuhumiwa waliofikishwa mahakamani na kutiwa
hatiani na wengine kuachiwa. Tume imeona kuwa hatua hii ilikuwa sahihi
kisheria. Lakini Tume ilibaini pia kuwa baadhi ya watuhumiwa
hawakufikishwa mahakamani.
Badala
yake maafisa wa Operesheni walijichukulia mamlaka ya kutoa adhabu kwa
watuhumiwa kama vile kukamata na kuzuia mali zao, kuchoma moto nyumba na
mali zilizokuwa kwenye maeneo ya hifadhi, kuua au kujeruhi mifugo
iliyokutwa kwenye maeneo ya hifadhi au kuuza kwa mnada ng’ombe
waliokamatwa kwenye maeneo ya hifadhi.
Hatua nyingine inayolalamikiwa ni kuchukua bunduki zinazomilikiwa kisheria.
5.8
Tume imebaini kwamba katika baadhi ya maeneo askari wa Operesheni
walichoma nyumba moto kwa madai ya nyumba hizo kujengwa kwenye hifadhi.
Malalamiko
hayo yalitoka katika Wilaya za Mlele na Mpanda, Mkoa wa Katavi, Wilaya
ya Momba, Mkoa wa Mbeya; Wilaya za Nkasi na Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa;
na Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara.
Katika uchunguzi wa matukio haya Tume imebaini yafuatayo:
- Wanakijiji hawakupewa taarifa ya kutosha kuhamisha mali zao kabla ya kuchoma nyumba zao;
- Baadhi ya wanakijiji walipoteza vyakula na mali zao katika zoezi hilo la uchomaji moto;
- Kuna vijiji vilivyosajiliwa lakini sehemu ya vitongoji vyake viko ndani ya Hifadhi za Taifa;
- Kuna maeneo ya hifadhi au ushoroba (buffer zone) ambayo hayana alama za mipaka kati ya hifadhi au ushoroba na vijiji husika;
- Kuna nyumba ambazo hazikuwa kwenye eneo la hifadhi au ushoroba na hivyo zilichomwa moto kinyume cha sheria.
- Baadhi ya matukio na malalamiko ya kuchomewa moto nyumba yalitokea kabla ya Operesheni.
5.9
Uchunguzi wa Tume umebaini kuwepo kwa tatizo kubwa la wafugaji kutoka
nje ya nchi na wafugaji wenyeji kuingiza mifugo yao katika Mapori ya
Akiba, Hifadhi ya Misitu, Maeneo Oevu na Hifadhi za Taifa.
Maeneo
yaliyoathirika sana na tatizo hili ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,
Pori la Akiba la Kigosi – Moyowosi, Pori la Akiba la Maswa, Mapori ya
Akiba ya Biharamulo – Burigi – Kimisi na Pori la Akiba la Kijereshi.
Katika baadhi ya maeneo imethibitika kwamba wapo ng’ombe waliouawa kwa kupigwa risasi baada ya kukutwa ndani ya hifadhi.
Aidha,
Tume imeridhika kwamba kuna ng’ombe wa walalamikaji waliokamatwa na
kuuzwa kwa mnada. Uuzaji wa ng’ombe katika tukio hili haukuzingatia
utaratibu wa kisheria.
5.10
Tume ilipata ushahidi kwamba katika maeneo mbalimbali askari wa
Operesheni walikamata au kuchukua bunduki, risasi pamoja na vitabu vyake
hata kwa silaha zinazomilikiwa kihalali.
Maeneo
ambayo yalikuwa na malalamiko ya watu kuchukuliwa silaha zao ni mikoa
saba (7) ambayo ni Katavi, Mbeya, Lindi, Morogoro, Tabora, Manyara na
Pwani ambapo jumla ya watu sitini na mbili (62) walijitokeza mbele ya
Tume kulalamika tukio hili.
6.0 Hatua Zitakazochukuliwa na Serikali
6.1 Baada ya kupitia kwa kina taarifa ya Tume, pamoja na mapendekezo ya Tume, Serikali itafanya yafuatayo:
6.1.1
Hatua za kimashtaka zitaendelea kwa shauri la mauaji ambalo upelelezi
wake umekamilika na hatua za kiuchunguzi zitaendelea kwa mashauri
mengine nane (8) ya mauaji ambayo upelelezi wake haujakamilika;
6.1.2 Hatua za kisheria na kiutawala zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa waliothibitika kuwatesa watu 15 wakati wa Operesheni;
6.1.3 Hatua za kiuchunguzi zinazofanywa na TAKUKURU kuhusu tuhuma za rushwa na udanganyifu zilizothibitika zitaendelea;
6.1.4
Silaha zinazodaiwa kumilikiwa kihalali zitafanyiwa uhakiki na ukaguzi
wa kina kuhusu umiliki na matumizi yake na endapo hakutakuwa na sababu
nyingine za kisheria za kuzuia urejeshwaji, wamiliki warejeshewe silaha
zao kwa mujibu wa sheria na taratibu;
6.1.5
Mali ambazo zimethibitika kuchukuliwa wakati wa Operesheni kwa tuhuma
za kuhusishwa na uvunaji haramu wa mazao ya misitu zirejeshwe endapo
hakutakuwa na sababu za kisheria kuendelea kuzishikilia;
6.1.6
Serikali itafanya uhakiki wa vijiji ambavyo vimesajiliwa na vimo ndani
ya hifadhi ili kutatua migogoro ya ardhi kati ya hifadhi na vijiji.
Aidha, Serikali itahakikisha kunakuwa na ushirikiano wa karibu kati ya
Msajili wa vijiji au mamlaka husika na Wizara ya Maliasili na Utalii
ili kuepuka kusajili vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi;
6.1.7
Wizara ya Maliasili na Utalii itatayarisha kanuni zitakazoweka
utaratibu wa kuwaondoa watu waliovamia na kujenga makazi katika hifadhi;
6.1.8
Sheria zote zinazolinda maeneo ya hifadhi zitafanyiwa marekebisho ili
kuongeza adhabu kwa kosa la kuingiza mifugo kwenye Hifadhi bila kujali
uraia wa wamiliki wa mifugo hiyo;
6.2
Kwa vile Tume imejiridhisha na faida kubwa na mafanikio ya
Operesheni Tokomeza, Serikali itaendelea na Operesheni kama hizo
kadri itakavyojitajika ili kuokoa maliasili za Taifa, ikiwemo
wanyama, hifadhi na misitu.
Hata hivyo ushauri wa Tume juu ya kuboresha upangaji, usimamizi na utekelezaji wa Operesheni hizo itazingatiwa kikamilifu.
7.0 Mawaziri Waliojiuzulu
Tume
ilijiridhisha kuwa Mawaziri wote waliojiuzulu, yaani Mhe. Dkt. Emmanuel
J. Nchimbi, Mb., Mhe. Balozi Khamis Kagasheki, Mb., Mhe. Mathayo D.
Mathayo, Mb., na Mhe. Shamsi V. Nahodha, Mb.,hawakuhusika moja kwa moja na makosa yoyote ya utekelezaji kwenye Operesheni Tokomeza. Hivyo, waliwajibika kisiasa tu na hakuna hatua nyingine inayostahili dhidi yao.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
8 Mei, 2015
Social Plugin