WAKATI mgomo
wa mabasi ukimalizika juzi, wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamekumbwa
na adha nyingine, baada ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kuleta
madhara mbalimbali kijamii na kiuchumi.
Katika maeneo mbalimbali ambayo waandishi wetu walitembelea leo, walikuta baadhi ya wakazi wakitoa maji yaliyoingia ndani ya nyumba zao na sehemu za kufanyia bishara zao.
Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Mwanayamala Mkwajuni maarufu kama
‘Bondeni’ wameonekana kutupia lawama Kampuni ya ujenzi ya Strabag kuwa
ujenzi wao wa barabara ndio umechangia nyumba zao kuingiliwa na maji
kwani mifereji iliyotengenezwa haikidhi uwezo wa kusafirisha maji kwa
kasi maana ni midogo, badala yake maji hujaa na kupitisha juu kuelekea
katika makazi yao.
Wakati huo huo waandishi wetu walifika maeneo ya Jangwani na kukuta
baadhi ya nyumba zilizoko bondeni zikiwa zimezama majini, huku
wakilalamika kutaka serikali iwasaidie, licha ya ukweli kwamba
walishaambiwa siku nyingi kuhama mabondeni.
Wakati huo huo, eneo la soko la Sinza-Afrika Sana, waandishi wetu waliwakuta wafanyabiashara ndogondogo wakilaumu mifereji inayopitisha maji barabarani kuziba kufuatia uchafu unaotupwa na kuziba maji kufika hadi sokoni hali inayopelekea biashara zao kudoda kutokana na wateja kukosa sehemu ya kupita.
Wakati huo huo, eneo la soko la Sinza-Afrika Sana, waandishi wetu waliwakuta wafanyabiashara ndogondogo wakilaumu mifereji inayopitisha maji barabarani kuziba kufuatia uchafu unaotupwa na kuziba maji kufika hadi sokoni hali inayopelekea biashara zao kudoda kutokana na wateja kukosa sehemu ya kupita.
Mvua
hiyo iliyofikia kipimo cha milimita 132.5 kwa mujibu wa vipimo
vilivyofanywa katika kituo cha Shule ya Msingi ya Maktaba, ilisababisha
barabara kujaa maji na nyingine kuharibika na madaraja kadhaa kukatika.
Mkurugenzi
Mkuu wa Hali ya Hewa, Dk Agnes Kijazi alisema jana kwamba kipimo hicho
cha mvua ni cha juu mno kulinganisha na kile cha wastani ambacho ni kati
ya milimita 16 na 30.
“Kwa
takwimu za mwezi Mei, kiwango hiki hakijawahi kufikiwa kwa miaka 10
iliyopita.” Alipotakiwa kufafanua miezi mingine, Dk Kijazi alisema
hakuwa na takwimu kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.
Awali,
Dk Kijazi alitoa taarifa ikisema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa
“hali ya mvua inatarajiwa kuendelea katika baadhi ya siku hadi Mei 20,
mwaka huu”.
“Mamlaka inaendelea kushauri wakazi wa maeneo hatarishi pamoja na watumiaji wa bahari kuchukua tahadhari,” alisema Dk Kijazi.
Watano wafa
Kutokana na mafuriko hayo, watu watano wakiwamo watoto wawili, walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji.
Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema waliopoteza maisha
ni watoto wawili na mzee mmoja ambao majina yao hayajafahamika.
“Mtoto
mmoja (2) alisombwa na mafuriko katika eneo Machimbo ya Makangarawe na
mzee mmoja alifariki jana baada ya mvua kunyesha na kujaa ndani ya
nyumba yake. Mtoto mwingine ambaye bado hajapatikana alisombwa na
mafuriko pia,” alisema Sadick.
Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye zilisema kuwa waliopoteza maisha ni watu watano.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alimtaja mtu
aliyefariki dunia kuwa ni Shabani Idd (73) mkazi wa Manzese.
Katika
eneo la Mbezi Luis, Mto Mbezi ulifurika, hali iliyosababisha nyumba
zilizojengwa kandokando ya daraja hilo kufunikwa na maji.
Mkazi
wa eneo hilo, John David alisema hali ilikuwa mbaya zaidi jana asubuhi
kwani maji yalifurika na kujaa barabarani na kusababisha usumbufu mkubwa
kwa watumiaji.
Alisema wakazi walio karibu na mto huo walichukua tahadhari tangu juzi na kuhama makazi yao.
“Haikuwa
rahisi kwa wao kuendelea kukaa hapa wakati wanafahamu hali kama hii
ingetokea. Tangu jana jioni familia zinazoishi huko ziliondoka, lakini
vitu vyao vimesombwa na maji na nyumba moja imesombwa pia,” alisema
David.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI UONE HALI INAVYOTISHA
Daraja la Kivule lilivyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar.Magari yakipita eneo hilo la daraja kwa tabu.Mkondo wa maji yanayopita darajani hapo.
Namna ambavyo soko la Sinza-Afrika Sana linavyoonekana kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar.
Mkazi wa Tandale kwa Tumbo akitoa maji yaliyojaa kwenye nyumba yake kufuatia mvua kali zinazoendelea kunyesha jijini Dar.
Wakazi
wa Tandale kwa Tumbo na maeneo ya jirani wakipita kwa tabu katika njia
hiyo kufuatia mvua ambazo zinaendelea kunyesha jijini Dar.