INAUMA sana! Katika kinachoonekana kama ni wivu wa kimapenzi, dada mmoja aliyefahamika kwa jina la Magdalena Lucas ( 23) ameuawa kikatili na ‘mumewe’ aliyetajwa kwa jina la Stephano Lucas (28) nyumbani kwao maeneo ya Mbezi Luis jijini Dar es Salaam wiki iliyopita baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani na mwili wake kufungiwa chumbani kwa siku tatu.
Mmoja wa majirani wa marehemu aliyejitambulisha kwa
jina la Benson Boaz alisema, imekuwa vigumu kwao kujua chanzo hasa cha
kifo cha msichana huyo aliyekuwa mfanyabiashara ndogondogo, ingawa
alikiri kuwa mara kwa mara wanandoa hao walikuwa wakizozana kutokana na
wivu uliokithiri wa mwanaume.
MUME ALIKUWA NA WIVU
“Mwanaume
ambaye alikuwa fundi ujenzi, alikuwa na wivu uliovuka kiwango kwa
Magdalena, alikuwa akimuwekea mipaka kuzoeana hata na majirani, huyu
kijana hakutaka na alipomuona mkewe anajichanganya na watu hakupendezwa
kabisa,” alisema.
Aliongeza
kuwa mara ya mwisho walimuona marehemu Ijumaa ya Mei 8 mwaka huu akiwa
na mumewe lakini hawakuwaona tena na hawakuwa na shaka kwa kuwa mlango
wao ulikuwa umefungwa kwa nje.
CHUMBA KUTOA HARUFU
“Jumapili
jioni tukasikia chumba chao kikitoa harufu kali, ndipo tukapata hofu na
kutoa taarifa polisi, walipofika na kuuvunja mlango, wakamkuta dada
huyo ameuawa, akionekana kupigwa na kitu kizito kichwani maeneo ya usoni
kiasi cha jicho lake kunyofoka. Hatujui kilichotokea maana hatukusikia
kelele huenda kwa vile mvua nyingi ilikuwa inanyesha na mwanaume
hajaonekana hadi leo,” alisema jirani huyo.
DADA HAMJUI SHEMEJIYE
Dada
wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Asteria alisema kifo
hicho ni pigo kubwa kwenye familia yao kwa kuwa tangu mdogo wake aanze
kuishi na Stephano, hakuwahi kuwaonesha ndugu zake.
“Tangu
mdogo wangu aanze kukaa na huyo shemeji, sisi ndugu hatukuwahi
kutuonesha tukamjua hata kwa sura, lakini majirani walijua kuwa ni mke
wake, naumia sana, ni bora asingeamua kuishi naye kwani hakuwa na upendo
wa kweli ndiyo maana kaweza kumfanyia ukatili wa aina hiyo,” alisema.
Marehemu
ambaye hakubahatika kupata mtoto, alizikwa katika Makaburi ya Tandale
kwa Ali Maua lakini ndugu na jamaa hawakupata nafasi ya kuuaga mwili
wake kutokana na kuharibika.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, ACP
Camillius Wambura alisema habari hizo hazijamfikia lakini atafuatilia
kwa kina tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake.
Credit: Gazeti la Uwazi
Social Plugin