JINSI MKUU WA WILAYA NA MAOFISA WA POLISI WALIVYONUSURIKA KUPIGWA MAWE JIJINI DAR ES SALAAM



MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na maofisa wa Jeshi la Polisi jana walijikuta katika wakati mgumu baada ya kunusurika kupigwa mawe na vijana waliokuwa wamejazana katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam.
 
Makonda na maofisa hao, walifika eneo hilo kwa nia ya kuwaomba madereva wa mabasi yaendayo mikoani kusitisha mgomo waliouanza juzi.
 
Maofisa wa polisi walionusurika kupigwa mawe ni Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura.
 
Tukio hilo lilitokea kituoni hapo saa 4:00 asubuhi, wakati Makonda alipokwenda kuzungumza na viongozi wa Chama cha Madereva kuhusu namna ya kumaliza mgomo uliodumu tangu juzi.
 
Makonda alipofika kituoni hapo, alikwenda moja kwa moja kufanya mazungumzo na uongozi wa madereva, huku akilindwa na askari polisi na wengine waliovaa kiraia.
 
Wakati mazungumzo yanaendelea, askari wengine walifika katika eneo hilo wakiwa na mbwa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.
  
Askari walianza kutumia mbwa kuwatishia madereva pamoja na umati mkubwa wa watu uliotaka kusikiliza kilichokuwa kikizungumzwa na baadaye mbwa alimrukia kijana mmoja na kumjeruhi mkono wa kulia.
 
Tukio hilo liliamsha hasira kwa baadhi ya madereva ambapo walianza kuzomea na kurusha mawe mfululizo katika eneo ambalo Makonda alisimama pamoja na maofisa wa polisi.
 
Hali hiyo iliwafanya viongozi wa polisi, wakiwamo Kamanda Mpinga, Wambura na wengine kujikusanya na kumkinga Makonda kwa kutumia mikono.
 
Kisha walifanikiwa kumweka chini Makonda ili mawe yaliyokuwa yakirushwa ovyo yasimfikie.
 
Watu wengine wakiwamo waandishi wa habari, walilazimika kukimbilia maeneo mengine ili kujinusuru na adha hiyo.
 
Vurugu hizo ziliwalazimu askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufyatua mabomu ya machozi na risasi za moto hewani ili kutawanya kundi kubwa la vijana.
 
“Hapa tumekuja kutafuta suluhu, wao wanatuletea mbwa na mabomu yao ya nini? Waandishi wa habari mnajionea wenyewe polisi ndio wanaoanzisha vurugu, si madereva,” alilalamika mmoja wa madereva hao.
 
Baada ya dakika kadhaa, Makonda aliendelea na mazungumzo na viongozi wa madereva hao.Makonda alisema anaunga mkono mgomo huo kwa sababu ni haki ya raia kudai haki yao.
 
“Mimi naunga mkono mgomo huu, kwa sababu ni haki ya kila raia na huu ndiyo msingi wa kupata haki yako kwa mtendaji asiyefanya kazi yake sawa sawa.
 
“Njia hii inasaidia kuwakumbusha viongozi kufikiri zaidi kwa niaba ya wale wanaowatumikia ili kutatua matatizo yaliyopo,” alisema Makonda huku akishangiliwa.
 
Baada ya Makonda kuzungumza hayo, Katibu wa madereva hao, Rashid Salehe, alisema lengo lao ni kutaka makubaliano yao na Serikali yawekwe kwenye maandishi.
 
“Si lengo letu kugoma kila mara, tunataka makubaliano tunayofikia yawekwe kwenye maandishi si kama vile alivyofanya Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) ili tukiona hayajatekelezwa tudai kwenda mahakamani,”alisema Salehe.
 
Baada ya kauli hiyo, Makonda alikubaliana na sharti hilo, hivyo alikwenda hadi katika ofisi za madereva hao kituoni hapo ili kuyaweka makubaliano hayo kwenye maandishi.

Katika Maongezi yake na madereva hao, Makonda alisema:“Tumeambiwa kwamba kuna tume imeundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, haiwezekani tume ikaundwa hewani, lazima tujue mambo matatu kuhusu tume hiyo.
 
“Lazima tuwajue viongozi waliomo ndani ya tume hii, muda ambao watafanya kazi yao na hadidu za rejea ambazo watazitumia.
 
“Lakini wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Ingawaje mnadai haki yenu nawasihi leo wapelekeni abiria hawa makwao, halafu kesho saa 4 nitaongozana na viongozi wenu kwenda kwa Waziri Mkuu tukajue mambo haya matatu kuhusu tume hiyo.”
 
Alisema iwapo watayaona majina ya wajumbe wa tume hiyo na kukosa imani nao, ataomba waongeze viongozi wawili wa madereva ambao wanawaamini.
 
“Iwapo leo hatutapata jibu katika madai yenu, nawaahidi nitakuja hapa na kuendelea na mgomo pamoja nanyi kwa muda wa siku saba hadi tupate mwafaka,” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post