Walikuwa wamevalia magunia, lakini sababu ya
kuvalia nguo hizo haikuwa kama maandiko hayo yanavyosema kuwa “kwa
sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu;
kwa maana hasira kali ya Bwana haikugeuka na kutuacha”.
“Tumejiuliza maswali mengi, tumeshindwa kupata
majibu. Tumejiuliza tuvae nguo gani hatukupata majibu. Kwa kuvaa hivi
tunataka hao wauaji wajue damu hii itawalilia popote walipo,” alisema
Beata Kiria, ambaye ni dada wa Victoria Sylvester aliyeuawa na watu
wasiojulikana na mwili wake kuzikwa nusu kiwiliwili.
Beata na ndugu zake walifika kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kuuchukua mwili huo wakiwa wamevalia magunia.
Tukio hilo lilitokea jana kati ya saa 4:30 asubuhi
na saa 6:00 mchana wakati ndugu hao walipofika chumba cha kuhifadhi
maiti cha hospitali, huku baadhi yao wakiwa pekupeku na kusababisha watu
wengi waliokuwa eneo hilo pamoja na watumishi wa hospitali kuwashangaa.
Wakiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti, ndugu
hao walilia wakipaza sauti wakitaka wauaji wa mwanamke huyo wakamatwe
kabla ya kuchukua mwili na kuondoka nao.
Victoria (53), mkazi wa Kijiji cha Masherini,
Umbwe eneo la Kibosho aliuawa kwa kukatwa mapanga usiku wa kuamkia
Ijumaa iliyopita na baadaye wauaji kuuzika mwili wake nusu na kuacha
kiwiliwili nje ya nyumba waliyokuwa wakiishi, jambo lililoibua utata
mkubwa ndani ya familia hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, Kiria alisema walichagua mavazi hayo baada ya kukosa vazi lingine.
“Tulitafakari tuvae nguo gani ili kumuenzi
marehemu lakini hatukupata jibu, ndiyo tukaamua tuvae magunia kuonyesha
kuwa waliomuua ndugu yetu thamani yao inafanana na magunia haya,”
alisema Kiria.
Imezoeleka misiba mingi ndugu huvaa suti nyeusi
kwa wanaume huku wanawake wakivalia mavazi meusi au meupe ambayo baadaye
hujifunika na vitambaa vyeusi au vyeupe kwa akina mama.
Kiria, ambaye alizungumza kwa niaba ya familia,
alilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linawatafuta na kuwakamata watu
waliohusika na mauaji hayo.
Social Plugin