Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amewajia juu Mkuu wa Wilaya ya
Rombo, Lemrise Kipuyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya hiyo,
Anthony Tesha akiwataka wajiuzulu nyadhifa zao kwa kushindwa kusimamia
sheria wilayani humo.
Selasini alitoa kauli hiyo jana alipokuwa
akizungumzia taarifa ya wanawake wa Rombo inayodai kwamba wanakodi
wanaume kutoka Kenya ili wafanye nao tendo la ndoa.
Juzi, gazeti la Mwananchi liliripoti habari iliyomkariri
Mkuu wa Wilaya kuwa baadhi ya wanawake wilayani humo, hukodi wanaume
kutoka Kenya kwa ajili ya kufanya nao tendo la ndoa baada ya waume zao
kupoteza nguvu kutokana na ulevi.
Eneo ambalo limeathirika zaidi na unywaji wa pombe
haramu na zinazotengenezwa kiholela bila viwango ni la Kikelelwa
lililopo mpakani mwa Kenya na Tanzania.
Taarifa hiyo ilimnukuu Kipuyo wakati wa ufunguzi
wa kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo na kuitaja Kikelelwa
kama eneo linalohitaji kutazamwa kwa jicho la pekee.
“Imefikia mahali wanaume wengi wanashindwa kumudu
kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu wanawake wao kukodi wanaume kutoka
nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya tendo hilo,” alisema Kipuyo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya wanawake
waliozungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya katika operesheni ya kukamata
pombe haramu ya gongo kijijini hapo iliyofanyika wiki mbili zilizopita.
Jana, Selasini alikanusha vikali taarifa hizo
akidai kuwa siyo sahihi kuwajumuisha wanaume wote wa jimbo lake na ulevi
huo au wanawake wote.
“Hiyo kauli haina utafiti wala haijaonyesha ni
wanaume wangapi Rombo wana tatizo hilo au ni wanawake wangapi waume zao
wana shida hiyo. Siyo sahihi kutoa kauli ya jumla,” alisema.
Alisema, “Haiwezekani mtu mmoja aliyehojiwa
akawakilisha wanaume au wanawake wenye matatizo hayo. Kauli hiyo
imewadhalilisha wanaume na wanawake ambao hawahusiki na tatizo hilo.”
“DC ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na
usalama aliyepaswa kusimamia sheria. Mwenyekiti wa halmashauri, naye
anawajibika. Kama wameshindwa kazi waachie ngazi.
“Siungi mkono unywaji holela wa pombe ambazo
hazina viwango vya TBS. Kama kuna mtu ana tatizo la tendo la ndoa
ajitokeza tumjue. Hili jambo limenifanya nipokea simu nyingi sana,”
alilalamika Selasini.
Selasini alisema inawezekana hakuna mwananchi wake mwenye tatizo
hilo kwa vile hakuna utafiti wala majina ya waathirika na alimtaka
Kipuyo kuomba radhi kwa kauli yake hiyo.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas
Gama naye aliwahi kutoa kauli inayofanana na ya Kipuyo aliposema wapo
baadhi ya wanandoa wilayani humo wanalala “mzungu wa nne”.
Via>>Mwananchi
Via>>Mwananchi