Vurugu kubwa zimetokea katika mji wa Njombe mkoani Njombe baada ya Basili Mwalongo mkazi wa mkoani humo kuuawa kwa kupigwa na polisi jana usiku ambapo wananchi wameandamana katika hospitali ya mkoa wa Njombe ambapo polisi wamelazimika kuwatawanya kwa risasi na kujeruhi wananchi kadhaa huku baadhi ya maduka yakifungwa na shughuli kusimama.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia wananchi wakiwa wameandamana na kufunga barabara huku wakiwasha matairi barabarani wakiwa wameshika chupa za maji kukabiliana na mabomu ya machozi ambapo amezungumza na majeruhi kadhaa wa kadhia hiyo Fredy Sanga akiwa amejeruhiwa kwa kupigwa risasi sehemu za siri na Lupiana Mandela aliyejeruhiwa kichwani.
Diwani wa kata ya Njombe mjini Bw. Agrey Mtambo aliyejaribu kuwatawanya wananchi hao bila mafanikio amesema purukushani kati ya polisi na wananchi ambapo polisi walianza kutumia silaha za moto.
Kufuatia vurugu hizo polisi mkoani Njombe wamelazimika kupiga mabomu ovyo kutawanya mikusanyiko ya watu huku kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Franco Kibona akigoma kuzungumza na waandishi wa habari kwa madai kuwa hawezi kuzungumza wakati vurugu zikiendelea halikadharika madaktari katika hospitali ya mkoa wa Njombe wakigoma kuzungumza.