Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

News Alert! MCHUNGAJI GWAJIMA AVAMIWA NA KUCHARANGWA MAPANGA NA KUPIGWA NONDO KICHWANI


MCHUNGAJI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima jijini Mwanza, Samson Gwajima na Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Amin Neigwa, wamevamiwa na majambazi ambao wamewajeruhi vibaya kwa kuwakata mapanga vichwani.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana katika Mtaa wa Lyila, Kata ya Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza.

Akizungumza kwa taabu na mwandishi wetu akiwa wodini kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC), alikolazwa kwa matibabu, Neigwa, alisema akiwa sebuleni nyumbani kwake na mkewe, ghafla walimuona msichana wa kazi aliyekuwa nje akichota maji, akiingia ndani kwa kasi na kukimbilia chumbani.

Alisema wakati akitahamaki kilichotokea, watu wanaosadikiwa kuwa majambazi waliingia ndani wakiwa na silaha za jadi kama mapanga, nyundo, vitu vyenye ncha kali na kutaka fedha.

"Walikuwa sita na baadhi yao walifunika sura zao kwa vitambaa, walinitaka niwape pesa...nilipata ujasiri wa kumrukia mmoja wao aliyekuwa na panga na kumkaba ndipo wengine wakanishambulia kwa kutumia silaha zao hadi nikapoteza fahamu," alisema.

Aliongeza kuwa, wakati wanamshambulia wengine walikuwa wanamlazimisha mkewe awape pesa lakini aliwakatalia na baadaye aliamua kuwapa sh. 10,000 ambayo ilikuwepo wakaichukua.

"Kelele nilizopiga wakati tumevamiwa zilisikika kwa majirani ambao walijitokeza ndipo wavamizi wakakimbia," alisema Neigwa ambaye alijeruhiwa kichwani ambapo hadi jana alikuwa akitokwa na damu masikioni.

Baada ya watu hao kukimbia, walienda kuvamia nyumbani kwa Mchungaji Gwajima na kumjeruhi kichwani kwa panga ambapo hivi sasa amelazwa katika hospitali hiyo kwenye Chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).

Mchungaji Gwajima ni kaka wa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, ambaye alivamiwa alipokuwa amelala na familia yake eneo la Lyila na kulazimishwa kutoa fedha.

Akizungumza na mwandishi wetu, Mchungaji wa kanisa hilo, John Kiula,  alisema Mchungaji Gwajima alivamiwa usiku ambapo baadhi ya mashuhuda walidai baadhi ya meno yake yameng'oka.

"Hadi sasa bado hajajitambua, tumetoka kwenye kipimo cha CT-Scan lakini majibu bado hatujapewa tumeambiwa yakiwa
tayari watatujulisha," alisema Mchungaji Kiula.

Mkuu wa Idara ya Dharura hospitalini hapo, Dkt. Derick David, alikiri kuwapokea majeruhi hao usiku na kusema Mchungaji Gwajima alifikishwa akiwa na hali mbaya zaidi kuliko Neigwa.

"Gwajima ana jeraha kubwa kwenye paji la uso ambalo ni kama sentimita mbili hadi tatu kwa urefu kwenda ndani, kipimo cha X-Ray kimeonesha hajapasuka mfupa ila hali yake si nzuri.

"Hadi sasa bado hajitambui, tunatarajia kumfanyia kipimo kikubwa cha CT-Scan ambacho kitaonyesha ameumia kiasi gani lakini Neigwa anaendelea vizuri ingawa naye anahitaji kupimwa na CT-Scan ili kuona majeraha yake kama amepata athari ndani ya kichwa, tunaendelea kuokoa maisha yao," alisema.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Naibu Kamishna wa Polisi, Charles Mkumbo, alikiri kutokea kwa matukio hayo na kuahidi kuyatolea ufafanuzi ambapo baadhi ya watu wamekamatwa wakihusishwa na matukio hayo.

"Mkuu wa Upelelezi Mkoa na timu yake walikuwa wanaendelea na uchunguzi, wakiukamilisha nitalizungumzia kwa undani na kuwataja walioshikiliwa, baadhi ya majambazi hao wametambuliwa na majirani,"alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com