Rais wa serikali ya Wanafunzi wanaosoma katika chuo kikuu cha Ushirika Moshi tawi la Kizumbi Shinyanga (MOCU) Bright Dominic Muro |
Rais wa serikali ya Wanafunzi wanaosoma katika chuo kikuu cha
Ushirika Moshi tawi la Kizumbi Shinyanga (MOCU) Bright Dominic Muro amewataka
watanzania kudumisha amani ya nchi ikiwemo kutowafanyia ukatili watu wenye
ulemavu wa ngozi (albino) kwa kuwakata viungo vyao.
Rais huyo wa MOCU ( Moshi Cooperative University) ameyasema
hayo juzi katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu wa ngozi cha Buhangija
katika manispaa ya Shinyanga akiwa ameambatana na wanafunzi wa chuo hicho
wakikabidhi msaada wa chakula na mahitaji mbalimbali muhimu kwa ajili ya watoto
hao.
Muro alisema amani ya taifa siyo tu taifa kuwa huru dhidi ya
vita wala mapigano bali ni watu wanaoishi katika taifa hilo kuwa na amani hivyo
kuitaka jamii kwa kushirikiana na serikali kupiga vita kwa nguvu zote mauaji ya
abino yanayowafanya waishi bila amani katika taifa lao.
Alisema amani kamili katika taifa ni pale watu katika jamii
wanapoishi na amani bila hofu yoyote na kuongeza kuwa amani ya Tanzania imeanza
kupotea kutokana na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi jambo linalosababisha
nchi ionekane kukosa amani.
“Tunalaani mauaji ya albino yanayoendelea nchini,sisi kama
serikali ya wanafunzi na sehemu ya jamii ya Tanzania tumeanzisha kampeni ya
kupinga mauaji ya albino,hata msaada tuliokabidhi umetokana na mchango wa
wanafunzi”,aliongeza Muro.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya mfuko wa kuchangia albino katika chuo kikuu cha Ushirika Moshi
tawi la Kizumbi Shinyanga (MOCU) Neema Medard Ngaita alisema mauaji ya albino
yanatokana na umaskini wa kifikra kwa baadhi ya watu kuamini kuwa viungo vya
albino vinaleta utajiri na vyeo.
Ngaita alisema ni vyema sasa jamii ikabadilika na kuachana
na tabia ya kuua albino na kila mtu katika jamii kuchukua jukumu la kuwalinda
watu wenye ulemavu wa ngozi.
Wakiwa katika kituo hicho wanafunzi hao walitoa misaada
mbalimbali ikiwemo unga wa sembe kilo 100,maharage kilo 100,unga wa lishe kilo
40,sabuni,madaftari,mafuta ya kula na kujipaka,kalamu,nguo na viatu vyote
vikiwa na thamani ya takribani shilingi 500,000/=.
Wanafunzi hao pia walishiriki shughuli mbalimbali ikiwemo
kufanya usafi wa mazingira na kufua nguo za watoto wanaolelewa katika kituo
hicho.
Akizungumza wakati wa kupokea misaada hiyo Mwalimu wa elimu
Maalum katika shule ya msingi Buhangija Sasu Nyanga kwa niaba ya mkuu wa kituo
cha Buhangija mbali na kuwashukuru wanafunzi hao pia aliitaka jamii kuendelea
kuwasaidia watoto wanaolelewa kituoni hapo ambao sasa wako zaidi ya 400.
Na Kadama Malunde-Shinyanga