Mbio
za urais ndani ya CCM sasa zimefikia pabaya baada ya kuibuka hofu ya
kuwapo kwa mpango wa kuivuruga Kamati Kuu kabla ya haijakutana kuchuja
majina ya makada watakaotakiwa kupigiwa kura na Halmashuri Kuu ili
kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi
Mkuu.
Hadi
sasa CCM haijatangaza ratiba yake kwa ajili ya kuongoza wanachama
wanaotaka kuwania uongozi wa ngazi mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho.
Hata
hivyo, Mwananchi ilitaarifiwa wiki hii kuwa Kamati Kuu ya CCM itakutana
Mei 20 na kufuatiwa na vikao vya siku mbili vya Halmashauri Kuu Mei 21
na 22 kwa ajili ya kupitisha ratiba, ilani na taratibu nyingine za
uchaguzi, ikiwa ni kuashiria kuanza rasmi kwa mchakato wa uchaguzi ndani
ya chama hicho kikongwe.
Wakati
chama kikitafakari kuanzisha rasmi mchakato wa uchaguzi, tayari kuna
habari kuwa moja ya makundi ya makada wanaowania urais limeonyesha
kutokuwa na imani na mwenendo wa Kamati Kuu ambayo ina jukumu la kuchuja
wanaowania urais na kupeleka majina Halmashauri Kuu kwa ajili ya
kupigiwa kura.
Taarifa
ambazo Mwananchi limezipata zinaeleza kuwa kundi hilo linashawishi
wanachama ili wakubali kuomba kupiga kura ya kutokuwa na imani na Kamati
Kuu kwa madai kuwa inaonekana kupendelea baadhi ya waliojitokeza na
kubana wagombea wengine.
Chanzo
chetu cha habari kimeeleza kuwa kundi hilo limekuwa likifanya vikao
mbalimbali vya kuweka mkakati wa jinsi gani ya kuivuruga Kamati Kuu
kabla ya kuchuja majina ya wagombea urais kwa tiketi ya CCM.
“Kuna
mkakati wa kuweka CC itakayowasaidia kwa kuwa ukishapita hapo,
umeshakuwa Rais wa nchi hii. Uzuri ukishinda ndani ya chama na
kutangazwa kuwa mgombea wao, basi makundi yote hurudi kukipigania chama
na wengine kujipendekeza ili wapewe nafasi katika serikali ijayo,” alisema mpashaji habari wetu ambaye ni mmoja wa viongozi wa juu wa CCM.
Taarifa
zaidi zinaeleza kuwa mpango huo unafanyika kwa umakini mkubwa ili
kuweza kuhakikisha Kamati Kuu haikati jina la mgombea wa kundi hilo kama
ambavyo imewahi kufanyika kwa makada wengine ambao majina yao
hayakupelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura kutokana
na nguvu yao kwenye chama.
Kama
hilo litafanikiwa itakuwa ni kwa mara ya pili kutokea baada ya mwaka
1995, Jakaya Kikwete kumlalamikia aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, Lawrance
Gama kuwa hawezi kumtendea haki baada ya kuonekana akiwa amevaa nguo
yenye nembo ya mmoja wa waliokuwa wakiwania kuteuliwa na chama hicho
kugombea urais.
Alipoulizwa
kuhusu mkakati huo, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema kuwa wamesikia na kuelezwa kuwa kundi hilo linagawa fedha
kufanikisha jambo hilo kwa kuwa wanadhani sekretarieti ya chama
haiwapendelei wao.
“Wanadhani
kuna watu wanapendelewa, kama suala hilo lipo bila shaka chama hakiwezi
kukaa kimya kwani huo ni uasi na usaliti kwa chama,”alisema Nape.
Alisema kuwa ndani ya chama viko vyombo vingi ambavyo kama mtu ana shida anaingia kwenye mikutano sahihi ya chama.
“Mtu huwezi kutengeneza vikao nje ya vikao halali halafu urudi kuongoza chama hicho hicho,” alisema Nape.
“Labda
watu wana mpango wa kukivuruga chama hiki halafu wagombee kwa chama
kingine sawa, lakini kama wanataka kugombea humuhumu CCM,
haitawezekana,” alisema Nape.
Mmoja
wa wajumbe wa CC ambaye pia ni Meya wa Ilala, Jerry Silaa alipoulizwa
kuhusu mkakati huo kama amesikia, hakuwa tayari kusema chochote kwa kuwa
yeye yupo ndani ya Kamati Kuu.
Hadi
sasa makada sita wa CCM wamefungiwa kwa zaidi ya miezi 12
kujishirikisha na harakati za uchaguzi ndani ya chama. Makada hao ni
mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Pia,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na waziri wa zamani wa Nishati na Madini,
William Ngeleja.
Baadhi
ya makada wanaotajwa kutaka urais kwa tiketi ya chama hicho ni pamoja
na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, waziri wa zamani wa Ulinzi, Emmanuel
Nchimbi, waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha na
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na Waziri wa Ujenzi, John Pombe
Magufuli.
Alipoulizwa
kama kuna watu wanapita kushawishi wanachama kujiunga na mkakati huo,
mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja alisema hofu hiyo
inatokana na chama kuchelewa kuruhusu wanachama wake kuingia kwenye
mchakato.
“Kama chama kingeruhusu mapema, kingedhibiti mapema mambo haya,” alisema Mgeja.
Muda
mfupi baada ya kumaliza mazungumzo, Mgeja, ambaye anaingia kwenye vikao
vya Halmashauri Kuu ya CCM kutokana na nafasi yake kwenye mkoa, alipiga
simu na kumweleza mwandishi kuwa anataka kuwatoa hofu wanachama wa CCM
kuwa chama kiko imara na hakuna ajenda ya mpasuko ndani ya chama.
Akizungumza
na gazeti la Mwananchi kwa simu, Makamba, ambaye ni mbunge wa Bumburi,
alisema amesikia kuwapo kwa mpango huo lakini hajathibitisha.
“Hata mimi nimezisikia habari hizo ingawa hazijathibitishwa. Kwa kuwa hazijathibitishwa, siwezi kuzungumzia kiundani,” alisema Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia.
“Nachoweza
kusema ni kwamba chama chetu kina utaratibu, kinatabirika na
kinaeleweka. Hakuna haja ya kuwa na papara katika hili na mimi sina hofu
na hili kwa kuwa najua kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa.”
Alisema
anajua kuwa uteuzi utafanyika miezi miwili kabla ya uchaguzi ili
utakapofika mwezi Agosti chama kipeleke majina kwenye Tume ya Uchaguzi
yakiwa yamechujwa kwa umakini bila ya kuwa na papara ya aina yoyote.
Waziri
Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ambao wote wanatajwa kuwamo
kwenye mbio za urais, hawakutaka kuzungumzia suala hilo, Membe akisema
yuko safarini kikazi na Sumaye akisema hajasikia habari hizo.
Juhudi za kumpata Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mbunge wa Monduli, Edward Lowassa hazikufanikiwa.
Credit: Mwananchi