Bajeti hiyo, imepitishwa leo mchana mjini Dodoma, baada ya wabunge kuipigia kura kwa kuitwa majina mmoja baada ya mwingine.
Akitangaza
matokeo hayo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, alisema wakati
upigaji kura unaanza, Bunge lilikuwa na wabunge 262, lakini walipokuwa
wakiendelea idadi iliongezeka kutoka idadi hiyo hadi kufikia 294.
Kutokana na idadi hiyo, alisema wabunge waliopiga kura ya ndiyo ni 219 na walioikataa ni wabunge 74.
Pamoja na idadi hiyo, alisema mbunge mmoja alitoa kauli iliyoonyesha hakushiriki kupiga kupiga kura.
“Wakati Bunge linaanza kupiga kura, ukumbini kulikuwa na wabunge 263,baadaye waliongezeka na kufikia 294.
“Wabunge
59 hawakupiga kura na waliopiga kura ya hapana ni 59,waliopiga kura ya
ndiyo ni wabunge 219 ambao ni sawa na asilimia 83.
“Pamoja na takwimu hizi, mbunge mmoja alisema ni abstain kwa maana kwamba hakukubali wala kuikataa bajeti,” alisema Dk. Kashilila ingawa hakumtaja mbunge huyo.
Lakini taarifa zinaonyesha ni Mbunge wa Mpanda Mjini,Said Amour Arfi (Chadema).
Pamoja
na matokeo hayo, kivutio kikubwa bungeni kilikuwa ni Mbunge wa Vunjo,
Augustine Mrema (TLP) kuikataa bajeti kuu ya Serikali kwa mara ya kwanza
tangu Bunge la 10 lilipoanza mwaka 2010.
Kitendo
hicho cha Mrema ambacho hakikutarajiwa, kiliamsha shangwe kutoka kwa
wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kwa kuwa waliamini
angeendelea kuiunga mkono kama alivyofanya kwa miaka minne iliyopita.
Pamoja
na Mrema, wabunge wengine waliosababisha kelele za shangwe bungeni
kutoka kwa wabunge wa CCM baada ya kupiga kura ya ndiyo ni Mbunge wa
Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid
Mohamed (CUF) na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP).
Wakati
bajeti hiyo ikipitishwa, baadhi ya wabunge wa upinzani walionyesha
kutoridhishwa nayo kwa kile walichosema kuwa haina jipya kwa vile
haiwalengi wananchi.
Akitoa
maoni yake kwa waandishi wa habari, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe, alisema bajeti hiyo ilipita kwa sababu kuna
wabunge wengi wa CCM.
Kutokana
na hali hiyo, alisema kuna haja ya wananchi kuwachague kwa wingi
wagombea wa upinzani, wakati wa uchaguzi mkuu ili Bunge lijalo
lisitawaliwe na chama kimoja kama ilivyo sasa.
Naye
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, kama alivyosema Mbowe, naye
hakuonyesha kuridhishwa na bajeti hiyo kwa kile alichosema haitaweza
kutekelezwa mwaka huu kutokana na uwepo wa uchaguzi mkuu.
Awali
akitoa ufafanuzi wa hoja za wabunge walizozitoa wakati wanachangia
bajeti hiyo iliyowasilishwa wiki iliyopita, Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya, alizungumzia tozo ya Sh 100 iliyopendekezwa na Serikali katika
mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.
Kwa
mujibu wa Mkuya, Serikali inatarajia kukusanya Sh bilioni 276 kutokana
na tozo hiyo na kwamba fedha zitakazopatikana zitapelekwa kwenye miradi
ya umeme vijijini na katika miradi ya maji.
“Lengo
la Serikali ni kuwapelekea wananchi umeme katika maeneo yao na ndiyo
maana tumeona ni bora wachangie shilingi 100 kwa kila lita ya mafuta
hayo.
“Kwa
kuwa lengo letu ni hilo, wenzetu wasiifanye kama hoja ya kujiongezea
umaarufu kwa sababu Sh bilioni 276, zitakapopatikana, Sh bilioni 90,
zitapelekewa kwenye miradi ya maji na zitakazobaki zitapelekewa kwenye
miradi ya umeme,” alisema Mkuya.
Kuhusu
malipo ya pensheni kwa wastaafu, alisema Serikali imeyaongeza kutoka
50,000 walizokuwa wakilipwa kwa mwezi hadi Sh 100,000.
Social Plugin