Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Laana Shinyanga_ BABA MCHEZA KAMALI ABAKA MTOTO WAKE WA DARASA LA PILI,AMHARIBU VIBAYA SEHEMU ZA SIRI


Mtoto ambaye jina limehifadhiwa mkazi wa kata ya Ngokolo mjini Shinyanga (10) anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Mapinduzi mjini humo, amedaiwa kubakwa na baba yake wa kambo Hatifu Hassan (30), na kumsababishia maumivu makali sehemu za siri.

Akielezea tukio hilo mama mzazi wa mtoto huyo jina limehifadhiwa alisema tukio hilo limetokea Juni 13, mwaka huu,majira ya asubuhi, ambapo yeye aliamka majira ya saa kumi 12 kwenda kwenye biashara zake za kuuza matango na kumuacha mume wake nyumbani, na muda mchache akapokea taarifa kutoka kwa majirani kuwa mtoto wake amebakwa.

Mama huyo alisema, baada ya kupokea taarifa hizo juu ya mwanaye kuwafanyiwa unyama na mumewake alirudi nyumbani na kumkuta mtoto wake ana hali mbaya huku akitokwa damu nyingi sehemu za siri pamoja na kinyesi kutoka hovyo, na kuamua kumkimbiza hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu.

“Nina mwaka mmoja naishi na huyu mwanaume ambaye anafanya kazi ya kucheza kamali, na mimi kazi yangu ni kuuza matango, ambapo siku hiyo niliamka alfajiri kama kawaida yangu nikaenda kwenye biashara zangu, mida ya saa tatu nikapokea taarifa kutoka kwa majirani kuwa mtoto wangu amebakwa.”alisema mama mzazi wa mtoto huyo.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga Salum Mfaume, alithibitisha kumpokea mtoto huyo majira ya saa tatu asubuhi siku ya tukio na kuanza kumpatia matibabu ,ambapo hivi sasa  hali yake inaendelea vizuri.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha  kuwa wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi na upelelezi ukikamilika atamfikisha mahakamani.
  
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com