WAZIRI wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, hivi punde ametangaza nia ya
kuwania urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa katika Viwanja
vya CCM mkoani Lindi.
Kauli mbiu ya kiongozi huyo ni ‘Twende na Membe kwa Manadiliko ya Uhakika’.
Katika hotuba yake, Mhe.
Membe amesema akipata fursa ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania anataka watoto wa Tanzania wawe wenye afya na wapate elimu,
wakina mama wasitembee umbali mrefu kufuata zahanati.
Pia amesema ataimarisha
ulinzi na usalama maana nchi ipo kwenye matatizo ya kiusalama kama
mauaji ya albino na madawa ya kulevya.
Katika sanaa na michezo,
Waziri Membe amesema amedhamiria kuondoa dhana ya kwamba Tanzania ni
kichwa cha mwenda wazimu katika michezo hivyo atahakikisha vyuo vingi
vya michezo vinafunguliwa pamoja na kutoa fursa kwa wanamichezo kwenda
nje ya nchi kupata uzoefu. Upande wa sanaa amesema atahakikisha wasanii
wanapata haki zao za msingi kama hatimiliki na kulinda kazi zao.
Aidha Waziri Membe
amesema akichaguliwa ataulinda na kuusimamia Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar maana ni wa kipekee duniani na ni tunu aliyotuachia baba wa
Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Membe ameongeza kuwa
akichaguliwa ataziunganisha sekta binafsi na za umma ili kukuza uchumi
na kuleta maendeleo sambamba na ajira.
Katika upande wa elimu,
Mhe. Membe amesema ataweka mkazo katika Shule za Ufundi na Veta kwa
kufufua vyuo vya ufundi maana ndiyo vinaongoza kwa kutoa ajira kwa
vijana.
Waziri huyo pia ameeleza nia yake ya kupambana na rushwa ili kuleta utawala bora nchini.
Social Plugin