Edward Lowassa |
Khamis Mgeja
Waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa kesho anatarajiwa kuwa
mgeni rasmi katika mchezo wa Hisani kati ya wakongwe (maveterani) wa soka wa Timu
ya Simba na Yanga kwa ajili ya kupata pesa kusaidia watoto wenye ulemavu wa
ngozi(albino) katika kituo cha Buhangija kilichopo katika manispaa ya
Shinyanga.
Mchezo huo umeandaliwa na taasisi ya Mzalendo Foundation
nchini inayojihusisha na Utawala Bora,Haki za binadamu,utamaduni na michezo utafanyika
kesho ,Alhamis ,Juni 11,2015 katika uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga
kuanzia saa 10 jioni.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo Khamis Mgeja ambaye pia ni
mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga amesema maandalizi ya
mchezo huo yameshakamilika na kuwataka wakazi wa Shinyanga na nje ya mkoa huo
kujitokeza kushuhudia mpambano huo na kuchangia watoto wenye ulemavu wa
Buhangija.
“Tumemuomba ndugu yetu Lowassa kuwa mgeni rasmi na amekubali
kuhudhuria,atakabidhi ngao kwa mshindi,hili zoezi litakuwa la wazi hakuna usiri
mapato yatakayopatikana ni kwa ajili ya kusaidia watoto albino”,ameongeza.
Aidha amesema mchezo huo utakuwa wa amani kulaani mauaji ya
albino na vyombo mbalimbali vya usalama vitakuwepo hivyo kuwataka watanzania
kujitokeza katika mchezo huo wa kuchangia watoto wenye ulemavu wa ngozi
wanaolelewa katika kituo cha Buhangija.
Amesema wameamua kuandaa mchezo huo wa magwiji wa soka kwa
ajili ya kutafuta pesa kwa ajili ya kuwasadia watoto wanaolelewa katika kituo
cha Buhangija wanaoishi maisha magumu wakikabiliwa na changamoto nyingi kubwa
zaidi ikiwa ni Chakula.
“Mzalendo Foundation inalaani vitendo vya kikatili dhidi ya
albino vinavyoendelea nchini hasa kanda ya ziwa ,katika mchezo huo wa
hisani,hapatakuwa na kiingilio chochote bali,mtu mwenye mapenzi mema na watoto
hao,atatakiwa kuja na mchango wa angalau kuanzia shilingi 1000/= tu na
kuendelea kama sehemu ya mchango kwa mahitaji ya watoto hao”,amesema Mgeja.
Katika hatua nyingine Mgeja ameiomba serikali kupitia wizara
zake kuangalia namna ya kusaidia watoto albino ikiwemo kutenga bajeti huku
akiwataka wabunge kuweka mkazo katika mambo yanayohusu walemavu wa ngozi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Soka mkoa wa
Shinyanga (SHIREFA) Benester Lugola amesema tayari wachezaji wa timu zote
wameshawasili mjini Shinyanga kwa ajili ya mchezo huo.
Amesema katika mchezo
huo hapatakuwa na kiingilio bali yeyote atakayeguswa na hali ngumu ya maisha ya
watoto hao anaweza kutoa chochote anachoona kinawafaa watoto hao.
Kituo cha watoto wenye ulemavu cha Buhangija hivi sasa kina
jumla ya watoto 396 kati yao albino 292,wasiiona 40 na wasiosikia 64 na
kutokana na ongezeko la albino kwa hofu ya kuuawa changamoto kubwa ni chakula.
Mahitaji mengine kwa watoto hao ni magodoro,vyandarua,vitanda,mavazi na mafuta maalumu kwa walemavu wa ngozi.
Na Kadama Malunde- Shinyanga
Social Plugin