Moja wa magari yaliyoharibiwa kwa kuvunjwa vioo likiwa limepaki katika ofisi za halmashauri ya mji wa Geita |
OFISA Uchaguzi pamoja na mwandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura
kwa mfumo wa BVR wamenusurika kifo baada ya kushambuliwa kwa mawe na wananchi wa
kituo cha Mwatulole Faziri Bucha katika kata ya Buhalahala Wilayani Geita
waliokuwa wakizuia mashine za BVR kuondoshwa kituoni ili hali wao
hawajaandikishwa huku risasi zikirindima kwenye kituo cha Shilabela katika kata
hiyo kuwatawanya wananchi waliokuwa wamewafungia maofisa uandikishaji ndani ya
kituo baada ya muda wa zoezi hilo kukoma.
Akithibitisha kutokea kwa vurugu hizo,kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita Hellen Kahindi aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na Utali Makweya(ofisa wa uchaguzi)aliyejeruhiwa kwa jiwe maeneo ya shingoni na Steven Oloo(mwandikishaji)aliyejeruhiwa mkononi.
Alisema maofisa hao walijeruhiwa jana majira ya saa 3 usiku katika kituo cha Mwatulole Faziri Bucha kata ya Buhalahala walipokwenda kwa ajili ya kuwaokoa wenzao pamoja na mashine za BVR waliokuwa wamezuiliwa kutoka kituoni hapo na wananchi ambao walikuwa hawajaandikishwa hadi zoezi hilo linamalizika jana majira ya saa 12 jioni.
Alisema wakiwa kituoni hapo wakati wakiingiza mashine kwenye gari gari ndipo wananchi hao kwa pamoja walianza kurusha mawe yaliyowapata maofisa hao ambao waliondoa gari kwa kasi kuokoa maisha yao huku gari moja la halmashauri hiyo lenye namba STJ 9519 aina ya Toyota Landcruser likivunjwa kioo cha nyuma na lile la idara ya usalama wa taifa ambalo namba zake hakuzipata mara moja likivunjwa vioo viwili vya ubavuni.
Aidha katika kituo cha Shilabela patashika la aina yake lilitokea majira ya saa nne usiku baada ya polisi kuamua kuwatawanya kwa mabomu ya machozi wananchi ambao walikuwa wamewafungia kwa nje baadhi ya maafisa uandikishaji wa kituo hicho wakiwashinikiza kuwaandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuwa jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa zoezi hilo kwenye kata hiyo wakipinga wao kukosa fursa hiyo.
Patashika hiyo ilichukua zaidi ya dakika kumi,kwani baadhi ya polisi waliokuwa na silaha za moto na mabomu ya machozi walifyatua risasi hewani kwa lengo la kutawanya vurugu hizo,na kufanikiwa kutuliza ghasia hizo.
Wakati hayo yanatokea wananchi hao walisisitiza kuwa kamwe hawezi kukubali kutokuandikishwa kwenye daftari hilo la Kudumu la Wapigakura kwani watakosa haki yao ya msingi ya kuchagua kiongozi wanayemtaka.
Hata hivyo, baadhi ya vijana walidai kuwa baadhi ya makada wa vyama vya siasa ikiwemo CCM ndio chanzo cha vurugu, kwani wameonekana wakisambaza makundi ya vijana ambo siyo wakazi wa eneo hilo kuandikishwa katika vituo mbalimbali huku wakazi wakikosa fursa hiyo.
Madai mengine yalikuwa mbali na NEC kuruhusu uandikishaji kuendelea hadi saa mbili usiku kutokana na wingi wa watu wanaostahili kuandikishwa lakini maofisa uandikishaji walifungua vituo hivyo majira ya saa 3 asubuhi hadi saa 12 jioni na ndiyo sababu wengi wa wananchi hawakupata fursa hiyo ya kuandikishwa.
‘’CCM wamekuwa wakileta watu ambao sio wakazi wa maeneo haya kutaka kujiandikisha hali ambayo imesababisha sisi wakazi wa eneo hili kukosa nafasi huku wengi waliojiandikisha ni kutoka maeneo mengine’’alisema James Felix Babileki(30)mkazi wa kata hiyo ambaye pamoja na kulala na kushinda kituoni toka zoezi lilipoanza hadi linamalizika jana kwenye kata hiyo hakupata fursa ya kujiandikisha.
Alisema hali hiyo ilitokana na kutokuwepo mabalozi kwenye vituo vya uandikishaji ambao ndiyo wenye jukumu la kujua mkazi wa eneo husika jambo lililosababisha wengi kuandikishwa kwenye maeneo yao mbali na kutokuwa wakazi na kusababisha msongamano usio wa lazima.
Baadhi ya vituo vilivyoathiriwa na msongamano wa watu kujiandikisha ili hali si wakazi wa eneo hilo ni pamoja na Magogo ambapo kwa mjibu wa mwenyekiti wa mtaa huo Paschal Mussa Nongo alidai kuwa mbali na mtaa wake kuwa na watu 580 waliofikia umri wa kupiga kura,waliojiandikisha ni 905 huku 48 ambao ni wakazi wa eneo hilo wakikosa fursa hiyo.
Malunde1 blog ilifika katika ofisi za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Joseph Konyo ili kupata ufafanuzi wa tukio hilo lakini hakupatikana baada ya kuelezwa na mmoja wa wasaidizi wake SP Bundala aliyedai yuko Mwanza kikazi na kumtaka mwandishi kuwasiliana na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Geita (RCO)SSP Pipi Kayumba aliyekuwepo eneo la tukio hilo.
Hata hivyo baada ya kumpigia simu hakukana wala kukiri na badala yake alisisitiza kuwa angelikuwa amepewa ruksa na kamanda mwenyewe angeweza kuzungumzia tukio hilo na kumtaka mwandishi ampigie kamanda ili ampe maagizo ya kuzungumzia tukio hilo lakini mwandishi alipomtafuta kamanda wa polisi simu yake ilikuwa imezimwa.
Hata hivyo katibu wa CCM Mkoa wa Geita, Gustavi Muba aliwataka wana CCM kutokuwa waoga na badala yake wajibu mapigo kwa kile alichodai vurugu zote zinaanzishwa na vijana wa Chadema kwa kuwazuia vijana wa CCM ili wasiandikishwe vinginevyo kwenye uchaguzi mkuu watashindwa.
‘’Wanaccm waache woga wakajiandikishe,hawa wenzetu chadema wanavurugu sana na wanawapiga vijana wetu nashindwa kuelewa kwa nini na wao wasijibu mapigo?wasipojibu mapigo tutachapwa kama tul;ivyochapwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa’’alisema Muba.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Geita Kahindi,baada ya zoezi hilo kumalizika kwenye kata hiyo Kesho(leo) zoezi hilo linatarajiwa kuendelea kesho katika kata ya kalangalala hadi juali 1 mwaka huu huku ukiwepo uwezekano wa kupeleka mashine kwenye kata ambazo zoezi hilo lilikwishamalizika ili kumalizia wale ambao hawakupata fursa hiyo.
Na Victor Bariety- Malunde1 blog Geita