TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
BASATA YAMJULIA HALI MSANII RAMADHAN MASANJA (BANZA STONE)
Timu ya watendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ikiongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Bi. Vivian Nsao Shalua mapema jana imemtembelea Msanii na mwimbaji wa muziki wa Bendi ndugu Ramadhan Masanja ‘Banza Stone” ambaye kwa muda sasa amekuwa akiugua nyumbani kwao maeneo ya Sinza Jijini Dar es Salaam.
Lengo la ziara hii ilikuwa kumjulia hali Msanii huyu mahiri wa Bendi na kushauriana na familia yake juu ya namna bora ya kusaidia matibabu yake na kuhakikisha anapata huduma zote stahiki kulingana na maelekezo ya daktari wake.
Katika ziara hiyo, watendaji hao wakiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) Mama Asha Baraka walipata wasaa wa kufanya mazungumzo na familia ya mwanamuziki huyo ili kupata maendeleo ya afya yake, matibabu na mwenendo wake.
Wanafamilia hao wa Msanii Banza Stone wakiongozwa na Kaka yake Khamis Ally Masanja walieleza kwamba hali ya mgonjwa huyo imekuwa ikibadilika mara kwa mara na kwamba amekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Sinza iliyoko Sinza Palestina jijini Dar es Salaam. Aidha amekuwa akipelekwa hospitali mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam ikiwemo ya Mwananyamala ambayo anaendelea kutibiwa kwa sasa.
Baada ya kupata taarifa ya kina kuhusu afya ya msanii Banza Stone, watendaji wa BASATA kwa kushauriana na wanafamilia hao walifunga ziara kwenda hospitali ya Sinza ambayo pia amekuwa akitibiwa na kufanya utaratibu wa matibabu ili kuhakikisha anapewa huduma stahiki na kuhakikisha afya yake inaimarika.
Akizungumza hospitalini hapo Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA Bi. Shalua alitoa wito kwa wadau wa Sanaa na wasanii kwa ujumla kumwombea msanii Banza Stone na kujitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha anarejea katika hali yake ya zamani na hatimaye kurudi kwenye Majukwaa ya maonesho.
“Wadau wa Sanaaa tumwombee na kumpa msaada stahiki msanii wetu. Msanii huyu ni muhimu kwenye tasnia ya muziki wa dansi. Amechangia sana katika kukuza muziki huu ndani na nje ya nchi. Tumwombee ili arudi katika hali yake ya awali” amesisitiza Bi. Shalua.
Imetolewa na Kitengo cha Habari cha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)