Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA vimetangaza rasmi kufikia makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Akitangaza makubaliano hayo mara baada ya kumalizika kwa kikao kirefu kilichokuwa kikijadili mustakabali wa kumpata mgombea urais pamoja na ugawanaji wa majimbo mapya, mwenyekiti mweza wa UKAWA James Mbatia amesema kuwa umoja huo umemteua mgombea ambaye ni chaguo la watanzania.
“Mgombea tutakayemtaja ndiye chaguo la watanzania” Amesema Mbatia
Mbatia amegoma kutaja jina la mgombea aliyepitishwa na umoja huo na kusema kuwa atatangazwa siku chache zijazo kwa madai kuwa anaandaliwa utambulisho maalum utakaoambatana na shamra shamra.
“Tayari jina tunalo lakini tutaliweka hadharani baada ya siku mbili tatu hivi, na tutamtoa kwa kimasomaso”
Katika kikao hicho kilichomalizika majira ya saa 3:30 usiku kikihusisha wenyeviti wa vyama hivyo pamoja na kamati ya ufundi ya UKAWA, mwenyekiti mwenza wa UKAWA kutoka chama cha wananchi CUF Prof Ibrahim Lipumba hakuweza kuhudhuria.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka CUF, chama hicho kilimuagiza Naibu Katibu Mkuu wa CUF Magdalena Sakaya kuiwakilisha, lakini baadaye Sakaya aliondoka katika kikao hicho bila maelezo yoyote.
Mkurugenzi wa mawasisliano wa chama hicho bwana Abdul Kambaya alipoulizwa kuhusiana na hilo akasema kuwa hakuna mwakilishi yeyote wa CUF aliyekuwepo kikaoni hapo hadi kikao hicho kikimalizika.
Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohammed alipoulizwa kuhusiana na kukosekana kwa Prof Lipumba kikaoni hapo amedai kuwa Prof Lipumba ni mgonjwa, na hali yake ya kiafya haimruhusu kuhudhuria kikao hicho.
“Mwenyekiti wetu ni mgonjwa, alikuwa safarini kutoka Kigoma, amerejea lakini hali yake si nzuri, ameshikwa na Malaria kali sana na miguu pia inamsumbua” Amesema Rajab Mbarouk.
Viongozi waliokuwepo wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari ni James Mbatia, Freeman Mbowe, Tundu Lissu, John Mnyika, Emmanuel Makaidi, Dkt Wilbroad Slaa, Dkt George Kahangwa (mgombea urais kupitia NCCR) na mtu anayetajwa kuwa mwakilishi kutoka chama cha CUF.
Katika hatua nyingine, afisa habari wa CHADEMA Tumaini Makene aliwaambia waandishi wa habari kuwa tayari vyama hivyo vimekamilisha kazi ya kugawana majimbo mapya 26 kazi iliyofanyika leo katika kikao hicho.
Kuhusiana na mgombea wa CCM Dkt John Magufuli, viongozi hao wamesema kuwa hawatishiki naye, na wala hawamfikirii, na kusisitiza kuwa mgombea ambaye ni chaguo la watanzania atatoka UKAWA na atatangazwa siku chache zijazo.
Via>>EATV
Social Plugin