Vurugu kubwa zimeibuka katika kituo cha kuandikisha daftari la kudumu la wapiga kura cha Fungafunga kata ya Kichangani manispaa ya Morogoro baada baadhi ya wananchi kuzuiwa kuandikishwa kwa madai kuwa si wakazi wa eneo hilo hali iliyosababisha mwenyekiti wa mtaa wa Fungafunga kupigwa na wananchi.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia vurugu zikiendelea katika kituo hicho huku afisa mtendaji wa kata ya kichangani Ashura Juma ameonekana akimshika kabali kijana aliyeanzisha vurugu ambapo ameeleza fujo hizo zimeanzishwa na kijana ambaye si wakala wa chama chochote alipoanza kupeleka watu kutoka nje ya mtaa na kutaka waandikishwe kwa nguvu.
Afisa mtendaji amethibitisha kupigwa kwa mwenyekiti wa mtaa kupigwa ngumi,makofi na kwamba vurugu hizo zimesababishwa na kijana huyo.
Kijana huyo aligombea Chadema uchaguzi uliopita akashindwa,wakati wa zoezi la uandikishaji akaanza kukusanya watu na kuwapeleka kuwaandikisha kwa nguvu tena siyo wakala na kusababisha vurugu hizo.
Wakieleza chanzo cha vurugu hizo mashuhuda na viongozi wa vyama vya siasa wamesema chanzo ni wafuasi wa chama cha Chadema kutaka waandikishwe watu ambao sio wakazi wa eneo hilo kinyume cha sheria huku mwenyekiti wa mtaa wa Fungafunga Ally Rashidi akieleza alivyopokea kipigo.
Katika vituo vingine wananchi wamelalamikia muda mchache wa kuandikishwa ambapo makamu mwenyekiti wa jumuiya wa wanawake wa chama cha wananchi CUF taifa Saverina Mwaijage wakati akitembelea vituo ameitaka tume ya taifa ya uchaguzi kuongeza muda wa kuandiksha kutokana na idadi kubwa ya wananchi ambao bado hawajajiandikisha kuhofia kukosa haki yao.
Via>>ITV