Viongozi wa Chadema wakiwa katika Kikao cha dharura cha Kamati Kuu.
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ametuma salaamu za pole na kuwatakia uponaji wa haraka majeruhi wa ajali mbili zilizotokea maeneo tofauti leo, moja ikihusisha helkopta nyingine ikitokana na ajali ya basi.
Chopa iliyokuwa imewabeba viongozi wa Chadema akiwemo Mbunge Nassari baada ya ajali.
Katika salaamu hizo, Mwenyekiti Mbowe ametoa pole kwa Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari, Mjumbe wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) Wilaya Eva Kaaya, Katibu wa Mbunge Elisa Mungure pamoja na rubani William Silaa kutokana na ajali ya chopa iliyotokea eneo la Leguruki wakati mbunge na viongozi hao walipokuwa kwenye ziara jimboni humo.
“Wakati tukiwa kikaoni hapa tumepokea taarifa mbaya zinazohusu ajali mbili, ajali moja imewahusisha Mbunge Nassari pamoja na viongozi wengine wawili wa chama ambapo chopa waliyokuwa wakitumia kufanya ziara jimboni kwake ime-crash.
“Taarifa za awali zimetuhakikishia kuwa wamenusurika katika ajali hiyo na wamekimbizwa Hospitali ya Serian mjini Arusha ambako wanaendelea kupata matibabu kutokana na majeraha waliyopata...hali zao zimeelezwa kuwa si mbaya sana.
Tunaendelea kufuatilia kwa karibu hali za majeruhi hao ambao wamepata ajali wakiwa kwenye mapambano.
“Mbunge wetu Mwanamrisho Abama naye amenusurika kwenye ajali iliyotokana na basi alilokuwa amepanda akiwahi kuja kwenye kikao hiki…basi hilo limepinduka wakati likitoka Dodoma kuja Dar es Salaam. Mheshimiwa Abama naye pia anaendelea vizuri.
Tuwatakie uponaji wa haraka wote waliopatwa na ajali hizo zote mbili na Mwenyezi Mungu awapatie wepesi katika hali hiyo,” amesema Mbowe.
Imetolewa 7 Julai 2015 na;
Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
Social Plugin