Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JINSI MBUNGE JAMES LEMBELI ALIVYOANGUA KILIO KWENYE MKUTANO WA CHADEMA




Mbunge wa Kahama, James Lembeli, ambaye hivi karibuni alitangaza kuihama CCM na kujiunga na Chadema, kwa mara ya kwanza amepokewa na umati mkubwa mjini Kahama hali iliyomfanya aangue kilio akiwa jukwaani.


Lembeli alisindikizwa na wabunge wa majimbo ya Mwanza waliomaliza muda wao, Haines Kiwia, Ezekiel Wenje na Mbunge wa Biharamulo, Anthony Mbasa katika na msafara wa magari, bodaboda na bajaji aliingia mjini hapa saa 9:30 mchana.


Lembeli na msafara wake walilakiwa na watu mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara waliosimamisha shughuli zao kwa muda huku wakionyesha alama ya vidole viwili ambavyo hutumiwa kama alama ya utambulisho ya Chadema


Katika msafara huo, wananchi hao walifunga barabara zote za mjini hapa hali iliyosababisha foleni ndefu hadi walipofika kwenye Viwanja vya CDT ambako mkutano huo ulifanyika.


Wakiwa katika mkutano huo Katibu wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Zacharia Thomas alimwelezea Lembeli kama mwanasiasa aliyekomaa ambaye nyota yake aliifukia jalalani lakini kwa kuhamia Chadema itang’ara zaidi.


Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Kiwia aliwataka wananchi wa Kahama pamoja na kumuunga mkono Lembeli wanapaswa kuwa na nguvu ya pamoja kuhakikisha kama atateuliwa na Chadema kuwania ubunge, wahakikishe wanalinda kwa nguvu kura.


Alisema Lembeli anaweza kushinda kwa nguvu kubwa Jimbo la Kahama lakini anaweza kuhujumiwa na wasimamizi wa uchaguzi ambao ni wakurugenzi wa halmashauri.


Kwa upande wake Lembeli aliyekuwa ameambatana na mama yake mzazi, Maria Kasembo alisema, uamuzi alioufanya ni mgumu lakini wizi na rushwa iliyokuwa ikifanyika katika ofisi za CCM ilimlazimu kuamua kuhama na kujiunga na Chadema.


Lembeli ambaye alikuwa akihutubia umati wa wananchi kwa kutumia kitabu cha Biblia alisema, uamuzi wake huo ni sawa na mwana aliyekuwa amepotea na sasa amerudi kuwakomboa wana wa Israel.


Alisema kuhama kwake kwenda Chadema atafanya kazi kubwa ya kutetea wanyonge kuliko alivyokuwa ndani ya CCM sehemu iliyojaa wizi na rushwa.


Hata hivyo, alipofikia kueleza kilichomtoa CCM, Lembeli aliangua kilio akisema pamoja na kufanya kazi kubwa hakupewa shukrani badala yake akawa mtu wa kuletewa wala rushwa na watoa rushwa ili wagombee ubunge kwenye jimbo lake la Kahama.


Pia, alisema pamoja na kugombea ubunge Kahama Mjini kama atashinda na kuwa mbunge atasaidia wananchi wa majimbo ya Kahama na Ushetu.


jimbo ambalo limezaliwa kutoka Kahama ambayo kwa pamoja ameyatumikia kwa miaka tisa na nusu na anajua matatizo yao.


Naye Mbunge wa Nyamagana aliyemaliza muda wake, Wenje alisema anamtambua Lembeli hata alipokuwa mbungeni misimamo yake ilionyesha kama mpinzani hivyo kuhama CCM ndipo atakavyofanya kazi vyema.


Wenje alisema Chadema hakuna mgeni mwanachama, yeyote akiingia leo anaanza kazi papo hapo hivyo Lembeli tangu siku aliyoingia alianza kazi ndiyo maana alikwenda Bunda kufanya kazi za chama hivyo Kahama wamuunge mkono.


Kwa kutumia mkutano huo, Lembeli alitangaza rasmi kuwania ubunge Jimbo la Kahama Mjini na kuwatoa wasiwasi wagombea wengine kwa madai demokrasia itazingatiwa wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya chama.

Na Shija Felician -Mwananchi Kahama

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com