Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu wanne akiwemo mwenyekiti wa mtaa wa Nyakato na kamanda wa sungusungu ambaye ni wakala wa UKAWA kwa tuhuma za kuandikisha wapiga kura kinyume na taratibu usiku saa nne na nusu katika mtaa wa Nyakato wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga na Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha tukio hilo limetokea Juni 30,2015 saa nne na nusu usiku katika mtaa wa Nyakato,kata ya Nyasubi wilayani Kahama.
Kamanda Kamugisha amewataja watu wanne waliokamatwa ni Nicholaus Kashanga Azalia Mbwambo( 40) mjumbe wa serikali ya mtaa wa Nyakato,Kamanda wa jeshi la jadi Sungusungu na wakala wa UKAWA katika zoezi la kuandikisha wapiga kura.
Wengine ni Amos Elias (25),mkazi wa Mhongolo( BVR Operator),Mayunga Alphonce( 54) ambaye ni mwenyekiti wa mtaa Nyakato na mkazi wa mtaa huo na Lugina Misango( 40) ambaye ni mratibu elimu kata ya Nyasubi.
Kamanda Kamugisha amesema watu hao wanaohojiwa na jeshi la polisi kuhusiana na tuhuma za kuandikisha wapiga kura kinyume cha sheria,ambapo watu hao wanatuhumiwa kuandikisha wapiga kura katika chumba anachoishi Nicholaus Kashanga Azalia Mbwambo kwa kutumia mashine moja ya BVR usiku.
Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo Kamanda Kamugisha amesema kaika mashine hiyo kumekutwa kadi tano ambazo zilikuwa zimechapishwa.
“Katika maelezo ya awali watuhumiwa wanadai mashine mbili zilipelekwa katika chumba hicho ambacho kiko katika nyumba ya Machanya Joshua kwa ajili ya kuchajiwa….”,ameeleza Kamanda Kamugisha.
“Pia tumemkamata Innocent Byamungu( 77) Mrundi ambaye baada ya kuhojiwa amedai kutoa Shilingi 5,000/= kwa Nicholaus Kashanga Azalia Mbwambo ili aandikishwe lakini hakuandikishwa kwa madai aliamuriwa na Nicholaus Kashanga Azalia Mbwambo aondoke kwa kuhofia kukamatwa”,ameongeza.
Katika tukio jingine watu wawili wamekamatwa na jeshi la polisi katika halmashauri ya mji Kahama kwa kosa la kuandaa na kuongoza maandamano yaliyohusisha vijana wapatao 80 wakipinga kuhamishwa kituo cha kuandikisha wapiga kura.
Kamanda Kamungisha amesema tukio hilo limetokea Julai 03,2015 saa nne na nusu asubuhi katika ofisi za mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kahama,ambapo Mary Issaack Sumuni(49) na Thobias Simon (36) wakazi wa Majengo walikamatwa kwa kuandaa na kuongoza maandamano hayo.
“Watu hawa waliandaa na kuongoza maandamano kutoka mtaa wa Majengo hadi ofisi za mkurugenzi bila kibali,walikuwa wanapinga kuhamishwa kituo cha kuandikisha wapiga kura kutoka Uwanja wa Halmashauri ya mji kupelekwa eneo la Maduka Kumi kwa madai kuwa watu wengi walikuwa bado hawajaandikishwa”,amefafanua kamanda Kamugisha.
Aidha amesema maandamano hayo yalisababisha kazi katika ofisi za mkurugenzi huyo kusimama kwa muda.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga anawaasa wananchi kufuata utaratibu uliowekwa na tume ya taifa ya uchaguzi katika kujiandikisha.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog Shinyanga
ANGALIA PICHA ZA TUKIO LA KUKAMATWA KWA MASHINE HIYO YA BVR HAPA