Mlinzi wa usiku katika Ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Florence Kazonde amejinyonga baada ya kumuua kikatili kwa kumkaba koo mkewe aliyekuwa na ujauzito wa miezi tisa, Emilia Mzui.
Chanzo cha mauaji hayo kimeelezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo limethibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani Rukwa, majirani na ndugu wa karibu wa familia ya marehemu hao waliokuwa wanaishi katika Kitongoji cha Namlangwa mjini Matai yalipo makao makuu ya wilaya ya Kalambo.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Halmashauri hiyo, Ramadhan Juma, alikiri kuwa Kazonde alikuwa mlinzi wa ofisi za Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo zilizopo nje kidogo ya Mji wa Matai, lakini hakuwa mwajiriwa wa halmashauri hiyo.
“Kazonde alikuwa anatoka katika kampuni moja ya ulinzi…hakuajiriwa na Halmashauri hii,“ alisisitiza Juma.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alieleza kutokuwa na taarifa za mkasa huo kwamba akizipata atazitolea taarifa.
Hata hivyo taarifa kutoka Jeshi hilo la Polisi mkoani humo limethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Kweli kuna hilo tukio limetokea wilayani Kalambo … taarifa zipo tayari lakini kwa kuwa mie si msemaji wa Jeshi hili siwezi kutoa maelezo zaidi ya kina lakini nikiri kuwa tukio hilo limetokea …
Kwa utaratibu wa Jeshi letu ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa ndiye msemaji na si vinginevyo.
Baadhi ya majirani na ndugu wa karibu kwa masharti ya kutoandikwa walieleza kuwa walibaini vifo hivyo baada ya kufika nyumbani kwa wanandoa hao ili kuwasabahi lakini walikuta milango ya nyumba hiyo imefungwa kwa ndani.
“..Tulihisi labda walikuwa bado wamelala lakini kila tukibisha hodi ni watoto tu waliokuwa wakiitikia …… “Mazingira hayo yalitutia mashaka makubwa tukahisi kuwa kwa kuwa mke wake siku zake za kujifungua zilikuwa zimekaribia tuliamini kuwa walikuwa wamekwenda hospitali na kuwaacha watoto wakiwa wamejifungia ndani na kushindwa kufungua milango hiyo, “ alisema mtoa taarifa.
Ilielezwa kuwa ndugu na majirani hao waliamua kufungua mlango kwa nguvu ili wawatoe watoto hao wadogo nje ambao walikuwa wawili.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa baada ya kufungua mlango wa nyumba hiyo kwa nguvu mmoja wa watoto hao aliwaonesha ishara kuwa chumbani kwa wazazi wao kuna kitu cha kutisha ndipo walipolazimika kuingia chumbani humo na kuona mwili wa Kazonde ukiwa umening’inia darini ukiwa na kamba ya katani shingoni ambapo mwili wa marehemu mkewe ulikuwa kitandani.
“Inatisha na kusikitisha sana ….tuligundua kuwa wote wawili walikuwa wafu tukatoa taarifa mara moja katika Kituo cha Polisi hapa mjini Matai …… askari Polisi walifika na waganga ambao walifanyia uchunguzi miili hiyo na kuthibitisha kuwa Kazonde alikuwa amejinyonga baada ya kumuua mke wake kikatili kwa kumkaba koo,” aliongeza mmoja wa ndugu wa karibu.
Taarifa kutoka eneo hilo la tukio zinaeleza kuwa kwa muda mrefu wanandoa hao walikuwa wakigombana mara kwa mara ambapo mume alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine na kwamba kati ya watoto wao wawili mmoja sio wake ni wa mwanamume mwingine.
Social Plugin