Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NANI MKALI KATI YA LOWASSA NA DR SLAA!!? MVUTANO WA URAIS TANZANIA WASHIKA KASI

Dk. Wilbroad Slaa (Kushoto) na Mh.Edward Lowassa (Kulia).

Zikiwa zimebakia siku sita kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumpata mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, kura ya maoni iliyoendeshwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia (REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inamweka kileleni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwa changuo la kwanza la wengi kwa kujipatia asilimia 27.0 ndani ya chama hicho.

Wakati Lowassa akiwafunika watia nia wenzake ndani ya CCM, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, anawafunika wenzake kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akiwa changuo la wengi kwa asilimia 23.1.

REDET wamesema kuwa matokeo ya utafiti huo yanaweza kuchukuliwa kwa ujumla wake kama maoni ya Watanzania endapo masuala yaliyoulizwa uchaguzi ungefanyika katika kipindi cha utafiti.

“Sampuli iliyotumika katika utafiti huu kwa kiwango cha kutosha ni wakilishi na ina akisi hali halisi ya Watanzania,” imesisitiza ripoti hiyo iliyojatwa kuwa ni maoni ya wananchi kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao wa Oktoba 2015, mwaka huu.

Katika utitiri wa watia nia ndani ya CCM, kati ya wahojiwa 1,250 waliohojiwa, Lowassa alipigiwa kura na watu 338, wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akipata asilimia 8.2 akichaguliwa na watu 103.

Utafiti wa REDET ulifanyika katika wilaya moja moja kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara baada ya wahojaji kukataliwa ruhusa ya kufanya utafiti wao katika mikoa mitano ya Zanzibar.

Utafiti huo uliokuwa umedhaminiwa na kampuni ya Business Times Limited, ulifanyika kati ya Juni 23-26, mwaka huu na kila wilaya ilikuwa na wahojiwa 50.

Kwa upande wa CCM watia nia wengine ni Mizengo Pinda nafasi ya tatu akiwa na asilimia 7.2 akichaguliwa na watu 90; John Magufuli nafasi ya nne akipata asilimia 6.6 akipigiwa kura na watu 83 na Charles Makongoro Nyerere nafasi ya tano akipigiwa kura na watu 54.

Wengine ni Mark Mwandosya nafasi ya sita akipata asilimia 3.1 akichaguliwa na watu 39; Dk. Harrison Mwakyembe nafasi ya saba akiwa na asilimia 1.4 akichanguliwa na watu 18; Frederick Sumaye nafasi ya nane akipata asilimia 1.4 akichaguliwa na watu 17; nafasi ya tisa imekamatwa na Jaji Augustino Ramadhani akiwa na asilimia 1.2 akichaguliwa na watu 15 na nafasi ya 10 amekamata Mwigulu Nchemba akiwa na asilimia 1.0 akichaguliwa na watu 13.

Wengine na idadi ya waliowachagua na asilimia zao kwenye mabano ni January Makamba nafasi ya 11 (asilimia 0.8, watu 10); Dk. Asha-Rose Migiro nafasi ya 12 (asilimia 0.7, watu tisa); Samuel Sitta nafasi 13 (asilimia 0.6. watu wanane); Lazaro Nyalandu nafasi ya 14 (asilimia 0.4, watu watano).

Pia wamo Prof. Sospeter Muhongo nafasi ya 15 (asilimia 0.4, watu watano); Balozi Amina Salum Ali nafasi ya 16 (asilimia 0.2, watu wawili); Dk. Mohammed Gharib Bilal nafasi ya 17 (asilimia 0.2, watu watatu); Stephen Wasira nafasi ya 18 (asilimia 0.2, watu 3) na William Ngeleja nafasi ya 19 (asilimia 0.2, watu wawili).

Wengine ni Balozi Ally Karume nafasi ya 20 (asilimia 0.1, mtu mmoja); Amos Siyantemi nafasi ya 21 (asilimia 0.1, mtu mmoja); Joseph Chagama nafasi ya 22 (asilimia 0.1, mtu mmoja); na Mwele Malecela nafasi ya 23 (asilimia 0.1, mtu mmoja).

Katika kura hiyo, watia nia 14 ambao wamejitosa kwenye urais kupitia CCM hawakutajwa kabisa na watoa maoni ambao ni Balozi Augustine Mahiga; Boniphace Ndengo; Eldophonce Bihelo; Godwin Mwaipopo; Dk. Hamis Kigwangalla; Dk. Hans Kitine; Joseph Chagana; Leons Mulenda; Luaga Mpina; Maliki Marupu; Mathias Chikawe; Monica Mbega; Titus Kamani na Balozi Patrick Chokala.

Kwenye kundi la Ukawa, namba mbili amechukua Prof. Ibrahim Lipumba akiwa na asilimia 13.6 akichaguliwa na watu 170; Freeman Mbowe ameshika nafasi ya tatu akiwa na asilimia 7.2 akichaguliwa na watu 90; James Mbatia amekamata nafasi ya nne akiwa na asilimia 3.2 akichaguliwa na watu 40; Emmanuel Makaidi akishikilia nafasi ya tano kwa asilimia 0.6 akichaguliwa na watu 8, huku George Kahangwa akishika nafasi ya sita kwa asilimia 0.2 akichaguliwa na watu wawili.

SWALI LA MSINGI
Swali la msingi lililokuwa linaulizwa lilisema: “Kama wewe leo ungeshirikishwa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, kati ya wanachama wake 37 waliokwishajitokeza, ungemchagua nani apeperushe bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 2015?”

Pia swali kwa Ukawa lilikuwa: “Kama wewe leo ungeshirikishwa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kati ya wanachama wake waliokwishakutangaza nia na wanaotarajia kutangaza nia ungemchagua nani apeperushe bendera ya Ukawa katika uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 2015?”

Ripoti ya REDET imesema kuwa kwa maswali yote, mhoji alitakiwa kutomtajia majina mhojiwa, bali mhojiwa aliombwa ataje jina alilonalo kichwani mwake.

REDET imesema kuwa katika utafiti wake ilikusudia kupata maoni ya wananchi katika maeneo matatu; mosi, kupata maoni ya wahojiwa kuhusu wanachama wa CCM wanaoomba kuteuliwa kuwania nafasi ya urais kwa tiketi ya chama hicho; mbili, kupata maoni ya wananchi kuhusu wanachama wa vyama vinavyounda Ukawa ambao wamejitokeza au wanafikiriwa kuwania nafasi ya urais chini ya mwavuli wa Ukawa na tatu, kupata maoni ya wahojiwa kuhusu wanachama wa vyama vingine vya upinzani vilivyo nje ya Ukawa wanaofikiriwa kwania nafasi ya urais.

Katika kundi la vyama ambavyo havipo Ukawa, Zitto Kabwe ameongoza kwa asilimia 8.5 akichaguliwa na watu 106, Chama cha Demokrasia Makini kimepata asilimia moja kilichaguliwa na watu 13, John Cheyo ameibuka nafasi ya tatu akiwa na asilimia 0.9 akichaguliwa na watu 12 na Augustine Mrema nafasi ya nne akiwa na asilimia 0.7 akichaguliwa na watu wanane.

Wengine ni Chama cha ADC nafasi ya tano kikiwa na asilimia 0.5 kikichaguliwa na watu sita na nafasi ya sita yupo Christopher Mtikila akiwa na asilimia 0.5 akichaguliwa na watu sita pia.

WILAYA ZA KURA YA MAONI
Wilaya ambazo kura ya maoni iliendeshwa ni Longido, Temeke, Dodoma Manispaa, Mbogwe, Kilolo, Muleba, Mlele, Ujiji Kigoma, Moshi Manispaa, Lindi, Hanang, Bunda, Rungwe, Morogoro Manispaa, na Msasi.

Nyingine ni Ilemela Manispaa, Ludewa, Kisarawe, Kalambo, Namtumbo, Kahama, Itilima, Singida, Tabora Manispaa na Muheza.

Ambako ruhusa haikupatikana ni Micheweni, Kaskazini B, Mkoani, Kusini na Mjini A.

VIJANA ZAIDI WAJITOKEZA
Katika utafiti huo ambao ulitumia mfumo wa sampuli nasibu (random sampling), vijana wengi zaidi walitoa maoni yao. Wahojiwa 334 sawa na asilimia 26.7 walikuwa kati ya umri wa miaka 36 – 45 na wengine 201 kati ya miaka 18 – 25 wakiwa ni asilimia 16.1. Wahojiwa wachache yaani zaidi miaka 66 walikuwa ni 70 sawa na asilimia 5.6.

Wanawake katika wahojiwa walikuwa 626 sawa na asilimia 501, huku wanaume wakiwa ni 624 sawa na asilimia 49.9.
Asilimia 30 ya wahojiwa wote walitoka mijini, huku asilimia 70 wakitoka maeneo ya vijijini.

VIPAUMBE SERIKALI AWAMU YA TANO
REDET wanasema kuwa wahojiwa walitakiwa kutaja kipaumbele kimoja tu na mlolongo uliopatikana ni elimu asilimia 23.8 iliyotajwa na watu 298; kilimo asilimia 14 watu 175, ajira asilimia 12 watu 150, afya asilimia 9.9 watu 124, kupambana na rushwa asilimia 6.4 watu 80 na maji asilimia 5.4 watu 68.

Nyingine ni barabara iliyoshika nafasi ya saba iliyopata asilimia 3.4 ikitajwa na watu 43, viwanda asilimia 3.3 ikitajwa na watu 41 na mikopo na mitaji asilimia 2.6 ikitajwa na watu 33.

Vipaumbelea vingine na asilimia na idadi ya waliotaja kwenye mabano ni umeme (asilimia 2.2, watu 28), kukomesha migogoro ya ardhi (asilimia 1.5, watu 19), ujenzi wa makazi/ nyumba bora (asilimia 0.6, watu 7), demokrasia (asilimia 0.6, watu 8), katiba inayopendekezwa (asilimia 0.3, watu watu 4) na muungano (asilimia 0.1, mtu mmoja).
CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com