Mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa wakati watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliposimamisha daladala eneo la Jangwani na kuingia ndani kupora mkoba unaosadikiwa kuwa na fedha.
Watu hao, waliokuwa na pikipiki aina ya boxer, walikuwa wakifuatilia basi hilo linalofanya safari zake kati ya Kariakoo na Mwenge na kulisimamisha eneo la Jangwani saa 7.30 mchana na baadaye kuwaamuru abiria wote wainame kabla ya kuelekea kiti cha nyuma alikokuwa amekaa mtu huyo aliyekuwa amebeba mkoba.
Mmoja wa abiria wa daladala hilo, Rehema Michael alisema wakati basi lao likiwa linaenda taratibu, alimuona mtu aliyekuwa amepakizwa kwenye pikipiki akishuka na kumfuata dereva na kisha kumuelekezea bastola usoni, akimtaka asimamishe gari.
Alisema dereva wao alitaka kukunja kona kuelekea Jangwani, lakini akatii amri na ndipo dereva wa bodaboda alipokwenda nyuma ya daladala na kumtaka mmoja wa abiria aliyekuwa amekaa nyuma ya daladala kutoa begi, huku mwingine akipiga risasi hewani, lakini hakupewa mkoba huo.
“Baada ya kuona yule abiria anakaidi agizo lao, mmoja wa majambazi hao alimpiga risasi ya kichwani na kifuani na kuanguka chini huku yule abiria mwenzake ambaye alipewa begi hilo alishike alilitupa chini na mmoja wa majambazi aliingia ndani ya daladala na kulichukua,” Hashim Ally.
Shuhuda mwingine, Richard Urio alisema wakati uvamizi huo ukitokea abiria walikuwepo ndani ya daladala hiyo akiwemo konda walilazimika kulala chini baada ya kusikia milio ya risasi zilizokuwa zikipigwa hewani, na kwamba baada ya kuchukua lile begi walimpiga risasi abiria mwingine ambaye alikuwa karibu na marehemu baada kuhisi alikuwa akizuia begi lisitolewe.
“Siti ya nyuma walikuwa wamekaa abiria wanne, na wawili kati yao walikuwa wamasai ambao mmoja wapo alikuwa amevaa begi mgongoni ambalo lilichukuliwa na majambazi baada ya kumuua mmoja wa wamasai huku mwingine akijeruhiwa na bastola shavuni,”Urio.
Shuhuda mwingine, Regina Mateso alisema yeye alipanda daladala hiyo eneo la Shakilango na kuwakuta wamasai hao ambao inasemakana walikuwa na fedha nyingi kutokana na maongezi yao.
“Wale wamasai walikuwa wanapigiana mahesabu na wapi kwa kwenda kubadilisha fedha. Yule aliyefariki alikuwa anamwambia mwenzake ukibadilisha hizi dola unapata Sh16 milioni, hivyo inawezekana wale abiria walikuwa na kiasi hicho cha fedha ambacho walikuwa wameweka katika begi la mgongoni,” Mateso.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Ilala, Lucas Mkondya alisema tukio hilo limetokea na wanalifanyia kazi .
“Na sisi polisi tumelipata sasa hivi ndio kwanza tunalifanyia kazi likikamilika tutatia taarifa,” Mkonya
Social Plugin