Umoja usio rasmi wa vyama vinne vya upinzani nchini Tanzania unajulikana kwa jina la Katiba ya Wananchi (UKAWA), baada ya kusubiri kwa muda hatimaye umemtangaza Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais.
Lowassa anagombea kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku vyama vingine vitatu vikimuunga mkono. Hii inatokana na sheria za Tanzania ambayo haitambui umoja wa vyama.
Kabla ya kujiengua chama Tawala chama cha Mapinduzi CCM, Edward Lowassa amekuwa mwanachama wa CCM kwa muda wa miaka 38, ambapo alijiunga na chama hicho mara tu baada ya kumaliza elimu yake ya chuo kikuu mwaka 1977.
Hatua ya mwanasiasa huyo mashuhuri nchini Tanzania kuamua kujiunga na chama cha upinzani Chadema, ikiwa imebaki miezi mitatu tu kuelekea uchaguzi mkuu, kumebadilisha kabisa upepo wa kisiasa nchini Tanzania, na hasa uchaguzi mkuu ujao.
Lowassa alikuwa Maziri Mkuu kati ya mwaka 2005 na 2008 kabla ya kujiuzuLu wadhifa huo kufuatia sakata la kashfa ya rushwa iliyohusisha kampuni ya kuzalisha umeme ya ki-Marekani Richmond Development Company LLC ya Houston Texas.
Hata hivyo wakati anatangaza kuhamia kwake Chadema, Lowassa alikanusha katu katu kuhusika kwa namna yoyote na kashfa hiyo na kudai kuwa yeye alifuata tu amri kutoka kwa ‘wakubwa’ walio juu yake.
“Kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi basi na aende mahakamani ama sivyo anyamaze” alisema Lowassa
Kuhama kwake kunamfanya Lowassa kuwa ndie kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kabisa wa CCM kukihama chama hicho tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mnamo mwaka 1992.
Mwanajeshi wa zamani na aliyewahi kupigana wa vita kati ya Uganda na Tanzania mwaka 1978/79, Lowassa aliiambia hadhara kwamba akiwa kama mtu mwenye uchungu na nchi yake isingekuwa rahisi kubaki ndani ya CCM huku akiona chama hicho kimepoteza mwelekeo na sifa ya kuongoza nchi.
Lowassa amekimbilia upinzani baada jina lake kukatwa wakati alipoomba kuwa mgombea urais kupitia chama tawala CCM katika uchaguzi mkuu ujao utakafanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Wakati mchakato wa CCM wa kumtafuta mgombea wao wa urais ulipoanza, Lowassa ndiye aliyekuwa kinara wa wagombea wote 42. Kila kona aliyozunguka, mikutano yake ya hadhara ilivutia maelfu ya watu waliomuunga mkono.
Wakati chama cha CCM kilimtaka kila mgombea apate sahihi za wadhamini 450 lakini Lowassa alipata sahihi za wadhamini zaidi ya 700,000.
Hata hivyo mchujo wa chama ulipofanyika jina lake lilikatwa mapema kabla hata ya kupelekwa kwenye vikao vya vya juu vya chama hicho. Ambapo baadae Waziri wa Ujenzi John Pombe Magufuli ndiye aliyeibuka kidedea na kuwa mgombea kupitia chama tawala CCM.
Lowassa ameushutumu mchakato CCM wa kutafuta mgombea urais akiuita kuwa ulijaa chuki na mizengwe dhidi yake, hali ambayo aliifananisha na ‘ubakaji wa demokrasia’
“Nitakuwa mnafki nikisema bado nina imani na CCM. CCM niliyoiona Dodoma si CCM niliyokulia”, alisema, na kuongeza “kama Watanzania hawapati maendeleo kupitia CCM basi wakayatafute nje ya CCM”
Wakati sakala la Richmond lilipoibuka miaka michache tu iliyopita, Chadema ilimfanya limsakama Lowassa kuwa ni mmoja wa mafisadi wakubwa nchini. Lakini wakati chama hicho kinamkaribisha kuwa mwanachama wao, kiligeuka na kusema hakuna mtu msafi nchini na kwamba hawawezi kuacha kumpokea mwanasiasa mwenye mtaji mkubwa wa wafuasi kama Lowassa.
Wakati akiwa Waziri Mkuu, Lowassa alisifika kama mchapakazi hodari na msimamiaji wa moja kwa moja wa shughuli za serikali. Bado anaendelea kufahamika kwa jina la utani la ‘mzee wa maamuzi magumu’.
Moja ya mafanikio makubwa ya uwaziri mkuu wake ni jitihada kubwa na mafanikio ya upatikanaji wa fedha za kujenga chuo kikuu cha Dodoma. Chuo hiki kikuu cha umma kilichopo katikati ya Tanzania kilianzishwa mwaka 2007.
Lowassa ni mashuhuri pia kwa kusimamia mpango wa serikali uliofanikiwa wa ujenzi wa shule za kata ambazo uliiletea Tanzania sifa kubwa kwa kutoa fursa ya watoto wengi kupata nafasi shuleni.
Mtoto wa Mzee Ngoyai Lowassa, ambaye aliwahi kuwa mtumishi wa serikali ya kikoloni, Lowassa ameanza harakati zake za kuwania urais tangu mwaka 1995 lakini inaarifiwa kwamba rais wa kwanza wa Tanzania Mwl Julius Nyerere alimkatalia kushika nafasi hiyo. Wafuasi wa Lowassa wamekuwa wakiyatupilia mbali madai hayo
Ulipofika uchaguzi wa mwaka 2005, Lowassa hakutaka kuwania urais, lakini badala yake alimnadi rafiki yake wa siku nyingi Rais wa sasa Jakaya Kikwete ambaye alipata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 80.
KWA KIFUPI HUU NDIYO WASIFU WAKE...
Edward Ngoyai Lowassa alizaliwa tarehe 26 August 1953, katika kijiji cha Ngarash wilayani Monduli mkoa wa Arusha, akiwa ni mtoto wa 4 kati ya watoto 23 wa mzee Ngoyai Lowassa.
Edward Lowassa amemuoa Regina Lowassa na kujaliwa kupata watoto watano, watatu wakiume na wawili wa kike.
ELIMU:
1961 - 1967: shule ya msingi Monduli
1968-1971: shule ya sekondari Arusha
1972 - 1973: St. Marry's High School (Milambo High School) Tabora.
1974 - 1977: University of Dar Es Salaam BA (Edu) Hons. Bachelor.
1983 - 1984: Chuo Kikuu cha BATH Uingereza M.Sc Masters Degree (Development Studies).
UZOEFU KAZINI:
1977-1978: Katibu Msaidizi ccm mkoa wa Shinyanga
1979-1982: Katibu Mtendaji ccm mkoa wa Arusha.
1983-1985 - Katibu mkuu msaidizi ccm Mkoa wa Kilimanjaro.
1985-1995 - Mbunge wa umoja Vijana wa ccm.
1989-1990 - Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha mikutano cha kimataifa (AICC) Arusha.
1990-1993 - Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu na makamu wa kwanza wa rais anayeshughulikia sera, Uratibu Bunge, Maafa namasuala ya mahakama.
1993-1995 - Waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya miji.
1995-2005 - Mbunge wa Monduli (ccm)
1995 - 2000 - Waziri nchi ofisi ya makamu wa Rais Mazingira, Muungano nakuondoa umasikini.
2000 -2005 - Waziri wa maji na maendeleo ya mifugo.
Desemba 2005 Februari 2008 Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
1985 - 2005 - Mbunge wa Monduli (ccm)
2010 - 2011 - Mwenyekiti Kamati ya bunge ya ulinzi na usalama na mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa .
2011 - 2015 - Mwenyekiti kamati ya bunge ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.
28/07/2015 - Kujitoa CCM na kujiunga na CHADEMA
Mhe. Edward Lowassa ni shabiki wa michezo na alikuwa mchezaji mzuri wa mpira wa kikapu.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin