Siku moja baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura za maoni ndani ya CCM na kushindwa, mbunge wa jimbo la Segerea Mheshimiwa Makongoro Mahanga ametanagza kukihama chama cha CCM na kujiunga na chama cha Chadema baada ya kutokutendewa haki katika mchakato huo.
Ukandamizaji wa demokrasia ndani ya CCM, ni moja ya sababu zilizomfanya naibu huyo waziri wa kazi na ajira kuamua kukikacha chama chake cha CCM, lakini wadadisi wa siasa za Tanzania wanabashiri huenda ukaribu wake na Lowassa ikawa miongoni mwa sababu kuu.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam Dkt Milton Makongoro Mahanga amesema kushindwa kwake kwenye kura za maoni kunatokana na hujuma na upendeleo uliofanywa na uongozi wa CCM wilaya ya Ilala kwa moja ya mgombea wa nafasi hiyo.
Anasema baada ya kujiridhisha na mbinu zote chafu zilizotumiwa na baadhi ya wagombea dhidi yake, na pia kujiridhisha bila shaka na namna viongozi wa CCM wanavyompiga vita tangu mwaka 2000 sasa anasema inatosha.
Katika mkutano huo pia amekiri kuwa na mahusiano ya karibu na waziri mkuu mstaafu Mheshimiwa Edward Lowasa na kwamba kama viongozi wa Chadema watamkubali anaamini atakuwa sehemu salama zaidi katika harakati zake za kisiasa hapa nchini.
Via>>Itv
Social Plugin