Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NI MARUFUKU KWA WANASIASA KUJIPITISHA NA KUFANYA KAMPENI HOSPITALINI


TAARIFA KWA UMMA UENDESHAJI WA KAMPENI ZA UCHAGUZI MAENEO YA UTOAJI HUDUMA ZA AFYA NCHINI


UTANGULIZI
Tumepokea taarifa kuwa wapo baadhi ya wagombea uongozi kuamua kutembelea Hospitali kama sehemu ya kuendesha kampeni za uchanguzi. Kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya huduma za afya, Hospitali ni sehemu inayopokea na kulaza wagonjwa wenye matatizo mbalimbali ya muda mrefu na muda mfupi. Pia yapo magonjwa yanayohitaji uangalizi wa karibu, na wakati mwingine huhitaji kutumiwa mitambo maalumu ya kuimarisha afya za wagonjwa.



Aidha, ikumbukwe kuwa katika mazingira ya sasa Duniani kote, Tanzania ikiwa ni mojawapo, yapo magonjwa mapya na yanayojitokeza upya (emerging and re-emerging diseases) ambayo mengine ni ya kuambukiza na ya milipuko.
Kutokana na hali hii wizara inapenda kutoa maelekezo kama ifuatavyo:-


Hospitali na vituo vingine vya kutolea huduma za Afya visitumike kwa madhumuni ya kuendeshea shughuli za kisiasa. Hii itasaidia kuzuia kupata magonjwa ya kuambukiza au kuingia hospitali na magonjwa ya kuambukiza. Hivyo ni vizuri kuchukua tahadhali kubwa hususan kipindi hiki ambacho kuna ugonjwa wa Kipindupindu.

Wizara inatambua umuhimu wa wagonjwa kutembelewa na ndugu na jamaa zao kwa lengo la kuwajulia hali. Katika mazingira haya utaratibu utaendelea kuwepo kama unavyofanyika nyakati nyingine kwa kuwa mgonjwa, anayo haki ya msingi ya kufarijiwa anapokuwa hospitalini na hata nyumbani, isipokuwa tu katika magonjwa ya kuambukiza.

Pale itakapoonekana kuwa baadhi ya wagombea wa nafasi za uongozi wana haja ya kutembelea hospitali kwa madhumuni tofauti na yale ya kuwajulia wagonjwa hali zao,itabidi waombe kibali maalumu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii . Wizara itakubali au kukataa maombi hayo kutokana na uzito wa ombi litakalowasilishwa pamoja na hali ya magonjwa yaliyopo katika eneo na hospitali au kituo husika cha kutoa huduma za Afya.

Tunapenda kusisitiza kwamba taarifa hii ina lengo la kuwazesha wagonjwa waliopo hospitalini kuendelea kupata huduma katika mazingira ya amani na utulivu. Hospitali na vituo vingine vya kutolea huduma za Afya nchini visitumike kama sehemu ya kuendeshea kampeni za siasa kwa vile ni maeneo maalumu ya kutolea huduma za Afya kwa mujibu wa Sera ya Afya na miongozo ya kutoa huduma za Afya.


IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
25/08/2015

Chanzo- Eddy blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com