Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe mama Salma Kikwete wakitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza la Kada Mkongwe wa CCM Marehemu Mzee Peter Kisumo wakati wa ibada ya mazishi iliyofanyika huko kijijini kwake Usangi- Mwanga Mkoani Kilimanjaro jana.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimfariji Mama Hosiana Kisumo Mke wa Marehemu Peter Kisumo wakati wa mazishi yake huko Usangi Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakiweka udongo katika kaburi la Kada Mkongwe wa CCM Marehemu Peter Kisumo wakati wa mazishi yaliyofanyika nyumbani kwake Usangi- Mwanga Mkoani Kilimanjaro.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo kilichowekwa kanisani wakati wa mazishi ya kada mkongwe wa CCM Mzee Peter Kisumo yaliyofanyika kijijini kwake Usangi-Mwanga Mkoani Kilimnjaro. (Picha zote na Freddy Maro)
Maziko ya mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo yametawaliwa na siasa za ‘chini chini’ kati ya makada wa CCM na wanachama wa Chadema huku Rais Jakaya Kikwete akishindwa kutoa hotuba.
Badala yake, salamu za Rais ambaye alikuwa rafiki wa karibu na marehemu zilitolewa kwa niaba yake na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha Rose Migiro.
Tukio jingine lililozua gumzo ni la makada wa CCM, wakiwamo viongozi waandamizi wa chama hicho kushiriki katika tukio la kumpokea Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa katika Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia).
Hata hivyo, makada hao ambao ni Katibu wa Uchumi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Paul Matemu na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM )wa mkoani hapa, Fred Mushi hawakufika kwenye maziko hayo yaliyofanyika Usangi.
Makada hao walikuwa katika msafara wa Lowassa ulioishia Mwanga baada ya kudhibitiwa na polisi.
Matemu alipoulizwa na kama ushiriki wake katika mapokezi ya Lowassa hauwezi kumletea matatizo, alisema siasa siyo uadui au uhasama na kwamba msiba hauna itikadi.
“Hivi tunapokwenda msibani ni marufuku wafuasi wa vyama viwili kupeana lifti au kwenda pamoja? Hivi nchi hii ndiyo imefika huko? Tukianza kubaguana kwenye misiba ni hatari,” alisema Matemu.
Awali, msafara wa Rais Kikwete uliwasili katika Uwanja wa Taifa ulio jirani na Kanisa Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kivindu, Usangi saa 9.20 alasiri kwa helkopta mbili zilizowasili kwa kupishana kwa dakika 12.
Akitoa salamu za Rais, Dk Migiro alisema Taifa linajivunia maisha ya Kisumo kwani alikuwa na msimamo thabiti katika masuala mbalimbali ya kitaifa.
“Aliyafanya hayo akilenga kuimarisha misingi ya utawala bora na alishiriki pia kutoa ufafanuzi wa kimantiki katika masuala mbalimbali wakati wa kuandika Katiba Mpya,” alisema Dk Migiro.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya familia ya Kisumo, Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya aliishukuru Serikali na Rais Kikwete kwa kugharimia matibabu ya Kisumo.
“Matibabu yake Kenya, Afrika Kusini na India yaligharimiwa na Serikali. Kila kilichotakiwa kufanywa na binadamu ili kuokoa maisha yake kilifanywa,” alisema Msuya.
Mwili wa Kisumo uliteremshwa kaburini saa 11.20 jioni na baadaye Rais Kikwete kuweka udongo kwenye kaburi la Kisumo ambaye aliwahi kuwa meneja wake wa kampeni mwaka 2005.
Katika ibada hiyo, makada wa CCM waliovalia mavazi rasmi ya chama hicho wakishirikiana na polisi, waliimarisha ulinzi huku vijana wa ulinzi wa Chadema wakidhibitiwa.
Mara baada ya vijana hao kuwasili katika viwanja vya kanisa hilo na kuanza kujipanga, maofisa wa polisi na wa CCM walionekana wakinong’onezana na kuonyesha vidole kuelekea kwa vijana hao.
Baadaye Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga alijitokeza na kutoa amri kuwa hawahitaji kusaidiwa ulinzi kwani wanao wa kutosha na kuwaamuru wakae kwenye viti kama waombolezaji.
Hali ya kuonyeshana ubabe haikuishia hapo, kwani baadhi ya makada wa Chadema waliokuwa wamevalia sare rasmi ya chama hicho walijikuta katika wakati mgumu wakitakiwa kuhama walipoketi.
Mmoja wa makada hao, Hawa Mushi aliamriwa kuondoka eneo la karibu na kilipowekwa kitabu cha rambirambi.
Viongozi wa upinzani walioshiriki maziko hayo ni Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema na mgombea urais kwa tiketi ya CCK, Dk Godfrey Malissa.
Chanzo-Mwananchi
Social Plugin