Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BASI LAUA WATU WATATU NA KUJERUHI ZAIDI YA 50 GEITA




Watu watatu wamefariki dunia na wengine 51 kujeruhiwa vibaya katika ajali ya basi Scania lenye namba za usajili T138 AVD, mali ya kampuni ya Sheraton.



Ajali hiyo imetokea baada ya basi hilo kuacha njia na kumgonga mwendesha bodaboda aliyekuwa amesimama kando kando mwa barabara kuu itokayo jijini Mwanza kwenda mkoani Kagera.


Tukio hilo la kusikitisha limetokea leo majira ya saa 3:30 asubuhi ambapo gari hiyo ilikuwa inatokea Masumbwe kwenda mkoani Mwanza baada ya tairi ya mbele upande wa kulia wa gari hiyo kupasuka na kupoteza mwelekeo na kupinduka ambapo abiria waliokuwa kwenye basi hilo wamesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari hilo.


Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Geita Dkt. Adam Sijaona amesema hali za majeruhi zinaendelea vizuri na kuongeza kuwa endapo kutakuwa na wakupewa rufaa watapewa na kwenda Bugando.



"Kweli nimepokea maiti tatu na majeruhi 51 kati yao bado hali zao ni mbaya na wengine wanaendelea vizuri ",alisema.



Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Geita Joseph Konyo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo huku akiwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuhakikisha wanavifanyia matengenezo vyombo vyao vya moto mara kwa mara ili kuepuka ajali zisizo za lazima.


Amesema jeshi la polisi linaendelea kufuatilia chanzo cha ajali hiyo.



Na Valence Robert Geita-Malunde1 blog Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com