Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM WAANIKA SIRI TANO ZA USHINDI KWENYE UCHAGUZI MKUU 2015



Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.



Wakati utafiti uliompa ushindi wa asilimia 65 mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, dhidi ya asilimia 25 za mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, ukipondwa na baadhi ya wasomi na wanaharakati kwa madai kuwa una kasoro kadhaa za kiufundi, CCM imeibuka na kufichua siri tano zinazowapa uhakika wa kushinda katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.



Juzi, Twaweza walitangaza ripoti ya utafiti uliohusisha watu 1,848 waliohojiwa kwa njia ya simu kati ya Agosti 19 na Septemba 17, mwaka huu na kuonyesha kuwa Magufuli angemuacha mbali Lowassa, anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).

Wasomi na wanaharakati mbalimbali waliponda utafiti huo kwa sababu mbalimbali, baadhi wakidai kuwa haujaeleza kwa uwazi sifa za watu waliohojiwa na wengine kueleza kuwa wiki mbili zilizopita tangu ufanyike hadi kutolewa matokeo yake juzi ni mrefu kiasi kwamba matokeo yake hayawezi kuakisi majibu halisi ya wapiga kura ikiwa uchaguzi ungefanyika sasa.

Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari jana, msemaji wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba, alisema wao wana uhakika kuwa chama chao kitashinda kutokana na mambo makuu matano.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za makao makuu ya CCM jijini Dar es Salaam jana, Makamba alisema jambo la kwanza linalowapa uhakika wa kushinda ni kitendo cha wapinzani wao (Chadema kupitia Ukawa), kuamua kumsimamisha kada wao wa zamani, Lowassa, kuwa mgombea wa nafasi ya urais.

"Sababu ya kwanza ni siku Ukawa walipomteua Lowassa kuwania urais. Hapo ndipo tuliamini CCM itashinda kwa sababu tunaamini hakuna namna Watanzania watamchagua (Lowassa)," alisema January.

Kwa mujibu wa Makamba, siri ya pili ya CCM ni kuendelea kwa matukio ya kujiweka kando kwa waliokuwa viongozi wakuu wa Ukawa, hasa Dk. Willibrod Slaa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema na mwenyekiti wa zamani wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba.

"Tuna amini migogoro hii ndani ya Ukawa katika kipindi hiki cha uchaguzi iliyosababisha kutokuwa na maelewano na pia viongozi wakubwa kujiuzulu... migongano iliyoko ndani ya NCCR-Mageuzi ni mfano mmojawapo. Haya yote yamepunguza imani ya wananchi kuhusu uwezo wa vyama hivi kushika dola," alisema.

Makamba aliitaja siri ya tatu kuwa ni kazi kubwa ya kujiuza kwa wananchi inayoendelea kufanywa na Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu.

Alisema wawili hao wamekuwa wakivutia maelfu ya watu katika kila mikutano na kufafanua vya kutosha kwa wananchi juu ya ahadi zao, ilani ya CCM na pia namna watakavyotekeleza kwa vitendo yote wanayoyaeleza.

"Wagombea wetu wamewafikia wananchi na wapiga kura wengi zaidi, hasa vijijini. Na wapiga kura hao wanawaelewa na kuwaamini, hivyo kampeni hizi zinazaa matunda na tuna amini tutashinda," alisema January.

Siri ya nne ya ushindi wa CCM, kwa mujibu wa Makamba, ni uungwaji mkono wanaoupata wagombea wao kutoka kwa wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge (wa CCM) waliopo karibu katika kila kata na majimbo ya uchaguzi nchini kote.

Jambo la tano linalowapa CCM 'jeuri' ya kuamini kuwa watapata ushindi mnono na kumtoa mrithi wa Rais Jakaya Kikwete baada ya uchaguzi mkuu mwezi ujao ni migogoro inayoendelea kushika kasi ndani ya vyama vinavyounda Ukawa, hasa juu ya nani agombee katika jimbo lipi kwani hadi sasa, kuna maeneo bado wangali wakivutana wenyewe kwa wenyewe kila uchao na kushindwa kupata muafaka, mfano katika majimbo ya Masasi mkoani Mtwara, Mtama (Lindi) na Temeke jijini Dar es Salaam.

Mbali na Lowassa, wagombea wengine watakaochuana na Magufuli siku ya uchaguzi ni Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Hashim Rungwe wa Chaumma, Fahmy Dovutwa wa UPDP, Chifu Lutasola Yemba wa ADC, Maximillian Lymo wa TLP na Janken Kasambala wa NRA.

USHINDI ZAIDI YA 60%
Katika hatua nyingine, Makamba alisema hadi kufikia jana, tafiti zao binafsi za kisayansi zinazohusisha utoaji wa ripoti kila wiki zinaonyesha kuwa Magufuli atashinda kwa zaidi ya asilimia 60 kwani tangu waanze kazi hiyo, hakuna wakati waliopata matokeo ya ushindi wa chini ya kiwango hicho.

Aidha, alisema CCM wananufaika na tafiti zao hizo za kisayansi kwa sababu kila wiki wamekuwa wakipata ripoti zinazowajulisha mwelekeo wa kampeni na maeneo yanayohitaji kuongezewa nguvu.

"Kuanzia sasa tutakuwa tunatoa taarifa kuhusiana na kampeni za wagombea wetu kila wiki na pia kuongeza kasi na mbinu zaidi za kampeni," alisema.


CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com