Wananchi wa wilaya ya Tunduru katika mkoa wa Ruvuma,wamemtaka mgombea urais kupitia chama cha ACT Wazalendo Anna Mghwira kuboresha huduma za afya katika mikoa ya pembezoni na miundombinu ya barabara katika wilaya hiyo ambayo wananchi wake hawaunganishwi kwa barabara za lami na wilaya jirani.
Wamesema wakati wa mkutano wa kampeni wa mgombea huyo wa urais,uliofanyika mjini Tunduru, kuwa wananchi wa wilaya hiyo hawana huduma stahiki kwa muda mrefu hivyo akiingia madarakani asaidie kutatua changamoto hizo,ambapo akihutubia katika mkutano huo wa kampeni amesema chama cha ACT Wazalendo kupitia ilani yake ya uchaguzi kitaboresha afya za wananchi wote kikianza na afya ya mama na mtoto.
Akizungumzia matumizi mabaya ya madaraka,amesema akipata ridhaa ya watanzania na kuwa rais atatumia sheria kuwawajibisha viongozi wote waliohusika na watakaohusika na ubadhirifu wa mali za umma huku viongozi wengine wa chama hicho wakiwataka watanzania kumchagua mgombea huyo wa urais kupitia ACT ili aweze kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Chanzo-ITV