ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ameibua siri nzito za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, na mkutano wake kurushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Channel Ten, Askofu Gwajima alisema kauli za Dk. Slaa si za akili yake anayoijua.
Katika mkutano huo, Askofu Gwajima alizungumza kwa kirefu kuhusu namna Dk. Slaa alivyoamua kujiondoa Chadema, baada ya kupigwa marufuku na mkewe, Josephine Mushumbusi kwa kile alichokiita nongwa ya mumewe kukosa nafasi ya kugombea urais.
Askofu Gwajima alisema tuhuma na kauli zinazotolewa na Dk. Slaa kwamba amejiondoa Chadema kwa kupinga ujio wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa si za kweli.
Alisema amekuwa na urafiki wa muda mrefu na Dk. Slaa hadi wiki iliyopita alipoamua kujiondoa kwenye ulingo wa siasa.
Askofu Gwajima, alisema Dk. Slaa alikuwa mtu wake wa karibu kiasi cha kufikia kutoa walinzi wake wawili ili wamlinde usiku na mchana pamoja na mfanyakazi wa ndani, Selina Mushi (50), ambaye alikuwa akimpikia chakula.
UJIO WA LOWASSA CHADEMA
Alisema ujio wa Lowassa ndani ya Chadema ambako anawania urais chini ya mwamvuli wa Ukawa, aliuanzisha Dk. Slaa mwenyewe baada ya jina lake kukatwa katika vikao vya chama chake cha zamani (CCM).
“Dk. Slaa alikuja kwangu nimuunganishe na rafiki yangu Lowassa kwa sababu ni mtu mwenye mvuto katika chama chake, jamii na ana nguvu kisiasa.
“Mimi ninataka nikiri nilifanya kila linalowezekana ili kuhakikisha Lowassa anakwenda Chadema… Dk. Silaa alivyoniita mshenga hakukosea, kwa sababu ninajua kila kitu. Mimi kusaidia kumleta Lowassa Chadema ni kazi ya Mungu, na Biblia inasema ‘heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu’.
“Mimi nilikuwa sahihi wakati ule kuwaleta pamoja wanasiasa hawa na kuafikiana hadi kufanya mikutano yao.
“Julai 26, mwaka huu siku ambayo Lowassa alipoingia Kamati Kuu ya Chadema pale Bahari Beach nilikuwapo hadi usiku wa saa sita, tulifanya mazungumzo kwa muda mrefu, niliomba kuingia huko ingawaje sihusiki, lengo langu ni kuhakikisha Lowassa anaingia Chadema salama na mimi nilikuwapo.
“Kikao hiki kiliisha saa 6:00 usiku na Lowassa alihutubia mkutano wake vizuri na alipomaliza, Dk. Slaa na mimi wote tulirudi nyumbani, usiku ule ule wa saa 7 nilipokea ujumbe mfupi wa maneno kutoka kwa mlinzi wa Dk. Slaa, Emmanuel, akisema kuna jambo limetokea usiku ule,” alisema.
MLINZI ATOA USHUHUDA
Baada ya kusema hayo, Askofu Gwajima alimuita Emmanuel ili aeleze kitu kilichotokea baada ya Dk. Slaa kufika nyumbani kwake.
“Siku hiyo, nilikuwa mlinzi wa zamu, nilipigiwa simu na mlinzi wa Chadema kuwa amemuacha Dk. Slaa njiani kwa sababu ya tatizo la usafiri.
“Tena kibaya Dk. Slaa alikuwa anaendesha gari mwenyewe, hivyo atakapofika nyumbani nimjulishe.
“Dk. Slaa alifika nyumbani, aligonga geti kuu na mimi nilimfungulia, nilimpokea mkoba wake kama ilivyo kawaida na aliuliza kama milango ya ndani ilikuwa wazi.
“Nilimjibu imefungwa kwa sababu ulikuwa ni usiku sana.
“Niliamua kwenda dirishani, nikamuasha mama, nikamwambia baba anaomba umfungulie mlango, mama alifungua mlango, huku akimwambia Dk. Slaa arudi alikotoka, kibaya kwenye kibaraza cha nje taa zilikuwa zimezimwa.
“Mama alifungua mlango, huku akiwa amebeba begi la nguo la Dk. Slaa na kulirusha na kumwambia arudi alikotoka… nikaona hii ni balaa.
“Nilihuzunika sana, niliondoka na Dk. Slaa tukarudi kwenye gari. Hapo ndipo alilala hadi asubuhi, niliamua kumtumia ujumbe mfupi wa maneno Baba Askofu Gwajima nikimweleza kuwa Dk. Slaa ametolewa begi la nguo nje na ameambiwa arudi alipotoka,” alisema.
KUTOKA CHADEMA
Askofu Gwajima ambaye katika mkutano huo alizungumza huku akisisitiza kuwa na ushahidi wa anachosema, alisema Dk. Slaa alimtumia ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu ya kiganjani aende nyumbani amjulie hali bila kumweleza kama alipata taarifa za yeye kulala ndani ya gari.
“Nilikwenda nyumbani kwake asubuhi, nilipofika alinikaribisha nikamuona akiwa mchovu sana…nikamwambia pole akanijibu nashukuru, nikamwambia usiku nilitumiwa ujumbe saa 7 nikamuonyesha namba na kumuuliza, je hii namba yako?
“Alinijibu kwa kusema ndiyo ya kwangu, nikamwambia jana ulinitumia ujumbe saa 7 usiku…akakiri kwa kusema kweli nimefungiwa ndani ya gari.
“Sababu kubwa ya kufungiwa ndani ya gari, nimetakiwa nijitoe kwenye siasa kuanzia sasa sababu familia yangu inavunjika,” alisema Askofu Gwajima.
Alisema baada ya kuambiwa maneno hayo na Dk. Slaa, kuwa mkewe amemwamuru aache siasa, alimtia moyo kwa kumwambia atamtafuta mkewe ili aweze kumshawishi amuache aendelee kufanya kazi ya siasa.
Huku akionyesha ujumbe huo wa simu aliodai kutumiwa na Dk. Slaa, Askofu Gwajima alisema: “Nataka Slaa akane meseji hii aliyonitumia saa 7:19 usiku ikiwa na namba yake, sasa atoke na kuikana kama si namba yake… halafu aone mambo ya mshenga yanavyoendelea.”
Alisema anasikitishwa na uongo wa Dk. Slaa anaodai amejitoa Chadema kwa sababu ya ujio wa Lowassa.
“Kauli za Dk. Slaa zinaonyesha wazi kujiondoa kwake Chadema hakukuchangiwa na ujio wa Lowassa, bali mkewe, Josephine ambaye tayari alikwishajiandaa kuwa mke wa rais.
“Ndiyo maana Watanzania mlio wengi, nikiwamo mimi, tunashangaa Dk. Slaa mpigania haki tuliyekuwa tukimjua na kile anachokifanya sasa kila mtu anashangaa… jamani tatizo ni mama.
“Ni mwongo kusema eti alihama Chadema kwa ajili ya ufisadi wa Lowassa no…ni uongo, ni uongo. Unajua Dk. Slaa alikuwa Padre, hana uzoefu wa ndoa, afadhali sisi wachungaji tuna uzoefu wa ndoa kwa sababu tunaoa, unaweza kujua namna ya ‘ku-manage’ ndoa yako,” alisema.
HARAKATI ZA KUMWOKOA DK. SLAA
Ili kuhakikisha anamsaidia Dk. Slaa aweze kurejea katika hali yake, Askofu Gwajima alisema alilazimika kumtafuta Josephine kwa nguvu zote ili waweze kuzungumzia na hatimaye amruhusu kuendelea na siasa.
“Nilimpigia simu na kumwomba tukutane pale Shekinah Garden, Mbezi Beach, tulifanikiwa kukutana jioni ya saa 12, nilitumia muda mwingi kumbembeleza nikimwambia tafadhali mama mruhusu huyo mtu aendelee na siasa, huku nikimrekodi, lakini alionekana kushikilia msimamo wake.
“Mama huyo aligoma kumruhusu kwa sababu eti ameandaa vitu vya biashara na ameshawaambia watu hata nje ya nchi kwamba ndiye atakuwa ‘First Lady’.
“Akahoji sasa watanionaje, nilikuwa nimepanga kuanza kufanya biashara Malaysia, mimi siwezi kukubali kabisa na sitakubali hata iweje,” alisema Askofu Gwajima huku akimnukuu Josephine.
Alisema: “Niliona jambo hilo ni gumu, yule mama pamoja na kumnunulia soda aligoma hali iliyofanya nimruhusu aende nyumbani.”
Askofu Gwajima alisema siku iliyofuata, yaani Julai 28, mwaka huu, alimpigia tena simu Josephine ili wakutane Kibo Complex, Tegeta wakiwa na mtu mwingine mmoja ambaye hakumtaja jina ili kumshawishi ajaribu kumnusuru Dk. Slaa asiharibikiwe baada ya kutokwenda Chadema.
“Tukiwa ndani ya gari yake, tukaanza kumwomba tena, nikajua tatizo linaweza kutokea nikawa narekodi tena. Safari hii mwenzangu alikuwa na huruma, akamwomba mama tusaidie huku tukijua siku hiyo Lowassa anakabidhiwa kadi ya Chadema pale Bahari Beach Hotel.
“Tulimwomba yule mama kuanzia saa 5:50 hadi saa 8 mchana, aligoma akimwambia yule mwenzangu kwamba ‘wewe umesahau hata kwenye jambo fulani mlipotaka kumwomba Dk. Slaa kwanza mlianza kuniomba mimi’. Yule mwenzangu akasema nakumbuka, nikajua tayari huyu mama ameshajenga msingi mbaya.
“Nawaonyesha hili, sio kwamba mumuone Dk. Slaa mbaya ila nataka niwaonyeshe alivyotekwa, mwenye nguvu ni mkewe, ilipofika saa nane mchana alikubali kumruhusu kurejea kazini kwa masharti.
“Kumbuka wakati ule Dk. Slaa ndiyo alikuwa anatakiwa kumpatia kadi Lowassa, mkewe alisema nimekubali, lakini ule mkutano wa Lowassa kupewa kadi leo ufutwe, mimi nitamruhusu aje… nikasema jambo hilo halipo jana, leo hata milele,” alisema Askofu Gwajima.
Baada ya kushindikana ushawishi huo, ilibidi wamtumie Mbunge wa Moshi Mjini aliyemaliza muda wake, Philemon Ndesamburo ambaye naye aligonga mwamba.
Alisema baada ya kuona mambo magumu, hakuishia hapo alimshirikisha kiongozi mwingine wa kiroho anayeheshimika nchini, Askofu Zakaria Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship.
Askofu Gwajima alisema Agosti 4, saa 12:30, akiwa na Askofu Kakobe walikwenda kumbembeleza tena Dk. Slaa, lakini mkewe aligoma na kung’ang’ania kwamba anachokitaka ni kuwa ‘First Lady’, huku akimtaka wazi kwamba mumewe asijihusishe tena na siasa.
MATUKIO YA AJABU
Katika hatua nyingine, Askofu Gwajima alisema mambo mbalimbali aliyoyahusisha na nguvu za ajabu, alikumbana nayo yote yakimuhusu Dk. Slaa na mkewe Josephine.
Alisema katika mambo hayo, kuna matukio manne tofauti ambayo yanajenga shaka juu ya maisha ya familia ya Dk. Slaa na mkewe kutokana na kutoa msaada wa maombi.
BOMU JINGINE
Askofu Gwajima, alisema endapo Dk. Slaa ataibuka kujibu hoja zake, atatoboa siri nyingine nzito namna alivyokwenda nchini Afrika Kusini hivi karibuni.
“Nasema kama Dk. Slaa akijaribu kujibu haya, nitatoa siri nzito namna alivyokwenda Afrika Kusini akiwa na watu wanne,” alisema Askofu Gwajima.
SHABANI MATUTU NA ASIFIWE GEORGE- MTANZANIA