Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LOWASSA AITEKA NGOME YA NAPE,MGEJA ASHANGAA PUSH UP ZA MAGUFULI..ADAI ANAFAA KUSHIRIKI OLYMPIC SIYO URAIS







Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, jana aliiteka ngome ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, Jimbo la Mtama baada ya kupata mapokezi makubwa katika mkutano wa kampeni.



Akiwa katika jimbo hilo la Mtama ambalo Nape pia anawania ubunge kupitia CCM, Lowassa anayeungwa mkono na vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema akishinda nafasi hiyo ya urais, ataunda tume ya uchunguzi kuhusu suala la mikataba ya gesi ili wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara wanufaike.

Aliyasema hayo wakati akizungumza katika mkutano mkubwa wa wananchi uliofanyika katika viwanja vya Majengo Jimbo la Mtama Wiilaya ya Lindi Vijijini.

"Gesi inatoka au haitoki?" Alihoji na kujibiwa kwa sauti kubwa kwamba `haitoki.'

Alisema akichaguliwa na kuwa Rais, ataunda tume ya uchunguzi kulifanyia kazi suala la gesi ili wananchi hao wanufaike badala ya raslimali hiyo kuwanufaisha wachache.

Mbali na gesi alisema atahakikisha elimu bora na bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu na kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana.

Alisema suala la kuwaondoa Watanzania katika umaskini ni moja ya sababu inayomsukuma kuutaka urais.

"Nimechoka na umaskini wa Watanzania, ninaamini ninaweza kuwaondolea Watanzania umaskini na kumfanya anayekula mlo mmoja aweze kula milo miwili," alisema.

Aliongeza kuwa ataboresha kilimo na kuruhusu wakulima kuuza mazao yao popote wanapopenda ndani au nje ya nchi bila kuwekewa vikwazo vyo vyote.

Akizungumzia mgogoro wa kumpata mgombea mmoja wa ubunge wa Ukawa katika jimbo hilo kati ya Isihaka Mchinjita (Cuf) na Mesi Selemani (Chadema), Lowassa alisema suala hilo litashughulikiwa na tume ya Profesa Baregu ambayo inapita kila jimbo lenye migogoro kutafuta muafaka.

SUMAYE: CCM IWATAJE WALIOTOROSHA TWIGA

Mapema, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alitaka CCM kuwaeleza wananchi nani waliohusika katika kashfa ya kusafirisha twiga na ujangili wa meno ya tembo.

Alisema CCM wanapaswa pia kutoa majibu ya tuhuma za biashara ya dawa za kulevya zinazokamatwa nje ta nchi zikiwa zimepitishwa katika viwanja vya ndege vya Tanzania na mzigo wa madeni badala ya chama hicho kuelekeza nguvu kupambana na upinzani.

"CCM watoe majibu na siyo kutuita sisi tuliokihama chama hicho kuwa tumechanganyikiwa," alisema na kuongeza CCM lazima kiondoke madarakani mwaka huu.

Alisema hata Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alikuwa muasisi wa CCM, alishawahi kutamka kwamba chama hicho siyo baba wala mama yake, hivyo kikikiuka misingi yake, anaweza kukihama.

"Halafu wapo watu wanasema tuchague CCM, hatuwezi kuendelea kuchagua CCM...chagueni chama kingine na kama baada ya miaka mitano mtaona hakijafanya vizuri, mtakuwa na uwezo wa kukiondoa madarakani," alisema Sumaye.

Aliongeza: "Sitaacha kuwatetea Watanzania hawa maskini ambao wameteseka miaka mingi...CCM waache kuwatisha wananchi," alisema.

Akifafanua kuhusu kura, Sumaye aliwataka wananchi kutunza vitambulisho vyao ili waweze kupiga kura kwani huo ni mkataba kati yao na chama.

Alisema CCM imewadanganya wananchi kwa kusema itawaletea maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini wameshindwa kufanya hivyo.

"Walituahidi maisha bora na ya raha, lakini tumepata maisha ya taabu na karaha," alisema na kutaja mifano ya ukosefu wa dawa hospitalini na huduma zingine za kijamii.

"Kuna sababu yoyote ya kuendelea kuichagua CCM iweze kushika madarakani, mnataka tuzame nayo wote?" Alihoji.

TAMBWE: MTOSENI NAPE
Kwa upande wake, Tambwe Hizza, alisema wananchi wa Jimbo la Mtama hawana sababu ya kumchagua mgombea ubunge wa CCM wa jimbo hilo, Nape Nnauye, kwa sababu hafai.

"Nape ni bingwa wa kuzalisha migogoro na matusi," alisema na kutaja baadhi ya migogoro hiyo kama ile ya sakata la Richmond pale alipowaita wenzake kuwa ni magamba.

Aliwatahadharisha kuwa akichaguliwa atazua migogoro na wenzake pamoja na halmashauri ya wilaya.

MGEJA ASHANGAA PUSH UP ZA MAGUFULI
Naye Khamis Mgeja, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, alisema anashangaa kuona mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli, akipiga push up, hivyo akasema anafaa kushiriki michezo ya Olympic na siyo kuwa rais.

Alisema mgombea ubunge wa CCM katika jimbo hilo, Nape anamfahamu na hajawahi kushinda uchaguzi wowote.

"Mna bahati mbaya sana hapa Mtama, sisi tunamwita .... amekumbuka shuka (kwao) wakati kumekucha," alisema na kuongeza Nape siyo mkazi wa Mtama na anakuja jimboni humo akiwa na brief case na kulala nyumba ya wageni kuomba kura.

Akimjibu Mzee John Malecela, aliyesema waliotoka CCM wana matatizo, Mgeja alisema waliotoka CCM ni watu safi.

"Sisi tuliotoka CCM ni watu safi kabisa, ukiwa mchafu CCM huwezi kutoka," alisema.

CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com