LOWASSA AZUA GUMZO KWENYE MKUTANO BAADA YA KUSEMA 'CCM OYEEEE",MWENYEWE ACHEKA


Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa jana alizua sintofahamu baada ya kusema;“CCM oyee”, kauli iliyowafanya wananchi hao kukaa kimya na walipoona akicheka waliitikia “oyeee” huku nao wakicheka na kumshangilia.



Ingawa ilitokana na ulimi kuteleza, yeye mwenyewe alisema alitamka neno CCM kama utani ili kubaini ni wananchi wangapi wanaokishabikia chama hicho kati ya waliojitokeza uwanjani hapo kumsikiliza wakati tayari amekwishaeleza jinsi chama hicho tawala kilivyoshindwa kuliletea taifa maendeleo.

Msindai kama Lowassa Wakati Lowassa akieleza kwamba alisema hayo kwa utani aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai aliyekihama chama hicho na kujiunga na Chadema, alitoa mpya baada ya kukiombea kura chama chake hicho cha zamani badala ya Ukawa kwenye mkutano wa hadhara.

Msindai alitoa mpya hiyo juzi jioni wakati akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni Jimbo la Manyoni Magharibi na Mashariki uliofanyika Manyoni mjini kwa tiketi ya Ukawa.

Baada ya kuwanadi wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani wa majimbo hayo, Msindai ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM Tanzania, aliwaomba wakazi wa Manyoni akisema: “Mpeni kura Lowassa ni mchapakazi na mwadilifu, anauchukia umaskini ataikomboa nchi yetu na kura zote za Rais, wabunge na madiwani wapeni wagombea wa Chama cha Mapinduzi.”

Baada ya tamko hilo, uwanja ulilipuka kwa kelele na minong’ono ndipo kiongozi mmoja aliponyanyuka na kwenda alipokuwa Msindai ameketi na ni kama alimwambia: “Hapa ni Ukawa si CCM.”

Alipopata maelekezo hayo, Msindai alisimama na kusema: “Ninaomba radhi, unajua koo limekauka, hebu kwanza naomba mnipe maji nipooze koo.”

Alipoletewa maji na kuyanywa, aliendelea kuomba radhi na kusema: “Ndugu zangu, ulimi uliteleza… si mnajua tumetoka huko hivi karibuni Uccm haujatutoka sawasawa,” alisema na kuamsha kicheko kwa mashabiki waliokuwa wakimsikiliza.

Msindai alikiri kuombea kura wagombea wa CCM kwenye mkutano wa Ukawa lakini alisema kuwa ulimi uliteleza na kwamba aliomba radhi na watu walimwelewa.

Hata hivyo, Msindai alikazia kusema kuwa Watanzania wanataka mabadiliko kwani hata mgombea wa CCM, Dk John Magufuli katika hotuba zake amekuwa akisema anataka kuona Tanzania ikibadilika.

“Watanzania watabadilika ikiwa Dk Magufuli atatimua watu wote kwenye mfumo wa utawala na kuleta mabadiliko ya kweli, lakini kama watu watabakia walewale, watamwangusha,” alisema Msindai.

Alipoulizwa utayari wa Watanzania kubadilika, Msindai alisema Ukawa ndiyo watakaoleta mabadiliko ya kweli kwa kuwa watawaondosha watu wote na kuleta watu wapya kwa ajili ya kufanya kazi,” alisema.

Alisema CCM ya sasa siyo ile ya (Julius) Nyerere na imebadilika na haitumikii tena wananchi na kwamba, Dk Magufuli ni mwenye hasira hivyo anakosa sifa. Mmoja wa makada wa Chadema Mkoa wa Singida, Paschal Mlaki alieleza kushangazwa na kuteleza kwa Msindai akisema ana wasiwasi na waliokuja kwenye chama hicho.
Chanzo; Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post