Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, jana aligeuka mbogo baada ya kuamua kuwataja hadharani watu wanaohujumu kampeni zake kwa kujifanya mchana wako pamoja na usiku wakigeukia upande wa upinzani.
Akiwahutubia wananchi wa mkoani Shinyanga jana katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage, Dk. Magufuli, alisema kuna mamluki wanaokihujumu chama hicho katika kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Dk. Magufuli aliwataja hadharani baadhi ya makada hao ambao wamekuwa wakiipigia kampeni CCM mchana na usiku wakiwapigia wapinzani.
“Kuna baadhi ya wana-CCM wanatujuhumu sana, wengine nawajua hata majina yao bahati nzuri huwa sisemi uongo bali ukweli, kuna huyu Gasper mchana tunakuwa naye CCM lakini usiku anaungana na wapinzani,” alisema.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Dk. Magufuli ilipokelewa kwa mshangao na baadhi ya wananchi na wanachama waliokusanyika uwanjani hapo, kwa kuwa baadhi ya makada hao walikuwa wameketi jukwaa kuu wakifuatilia hotuba yake.
Waandishi wa habari hizi walimshuhudia meneja kampeni wa mgombea huyo, Abdallah Bulembo, akimfuata Magufuli na kumnong’oneza ,ghafla Magufuli alibadilisha na kudai msaliti ni Gasper Anthony wala si Gasper Kileo aliyetajwa awali.
Hata hivyo, Magufuli baada ya kumaliza hotuba yake alimfuata kada wa CCM mkoani Shinyanga anayetumia jina la Gasper aliyeonekana kupaniki na kumkumbatia huku akimtuliza na kuendelea na msafara wake.
Kwa upande wake Mjumbe wa NEC anayetumia jina la Gasper alipopigiwa simu yake ya mkononi na mwandishi wetu kumzungumzia tuhuma zilizoelekezwa kwake kuwa ni msaliti ndani ya Chama simu yake haikupatikana.
Awali wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais wa CCM MNEC Gasper Kileo alikuwa ni miongoni mwa makada wa CCM ambao walikuwa wakimuunga mkono Edward Lowasa lakini baada ya kukatwa jina lake, na kuamua kuhamia Ukawa, Gasper hakuweza kuhama na kubakia CCM.
Hata hivyo wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi CCM mkoa wa Shinyanga hivi karibuni Gasper Kileo aliwataka wananchi kupuuza uvumi kuwa anaendelea kumuunga mkono Edward Lowassa baada ya kuhamia Ukawa.
Kileo alisema hajawahi kufikiria na wala hafikirii kuhama CCM hivyo ataendelea kuunga mkono CCM na kuahidi kushiriki kwa hali na mali katika kuijenga CCM huku akidai kuwa anamuunga mkono mgombea urais wa CCM John Magufuli na kuomba wakazi wa Shinyanga kumpa kura mgombea huyo.
WAANDISHI WAKUMBANA NA VIKUMBO
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida waandishi wa habari mkoani Shinyanga walikumbana na vikumbo vya hapa na pale na baadhi ya makada wa CCM na baadhi ya waandishi wa habari waliopo kwenye msafara wa Magufuli waliodai kuwa waandishi ambao hawapo kwenye msafara kuwa hawaruhusiwi kupiga picha wala kuandika habari za katika kampeni za Magufuli.
Waandishi wa habari licha ya kuwa na vitambulisho vya kazi walikatazwa kupiga picha za mkutano huku sababu za kuwazua zikitajwa kuwa wanaopaswa kupiga picha ni waandishi walioko kwenye msafara pekee kwani wamepewa utaratibu wa kufanya kazi kwenye mikutano.
Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya Magufuli kumtaja Gasper kuwa ni mmoja wa wasaliti wa CCM,baada ya wandishi hao kumpiga picha akiwa jukwaa kuu,ambapo waandishi waliondolewa eneo la mkutano huku wakitishiwa kupigwa kisa kwanini wanampiga picha Gasper.
Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya Magufuli kumtaja Gasper kuwa ni mmoja wa wasaliti wa CCM,baada ya wandishi hao kumpiga picha akiwa jukwaa kuu,ambapo waandishi waliondolewa eneo la mkutano huku wakitishiwa kupigwa kisa kwanini wanampiga picha Gasper.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga Kadama Malunde ambaye ni miongoni mwa waliopata msukosuko wakati akimpiga picha kada wa CCM anayetumia jina la Gasper alisema kitendo cha kuzuia waandishi wa habari kufanya kazi yao ni kuwanyima uhuru waandishi wa habari hivyo ni vyema wagombea wakawaeleza makada wao hasa Greenguard kutambua uwepo wa wana habari badala ya kutambua walioko kwenye msafara pekee.
"Tunalaani kitendo cha baadhi ya WanaCCM na baadhi ya waaandishi walioko kwenye msafara kuzuia waandishi wasiokuwa kwenye msafara kutofanya kazi yao,inavyoonekana waandishi wamenunuliwa,huwezi kusema kuna utaratibu wa kuandika habari za mgombea flani,Hii hali itatugawa waandishi wa habari Tanzania,Naomba mamlaka zinazohusika waliangalie suala hili kwa umakini zaidi",alisema mwenyekiti huyo.
Akiwahutubia mkoani Shinyanga, Magufuli amesema hashangai wananchi kuanza kumwita rais kwasababu hata yeye anajua kuwa ndiye atakayeibuka na ushindi mnono kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema wagombea wengine wa nafasi ya urais ni wasindikizaji tu kama walivyo wapambe wa kwenye harusi.
Na Waandishi maalumu wa Malunde1 blog Shinyanga