Mkutano wa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, katika jiji la Tanga jana ulikumbana na balaa la aina yake baada ya watu kadhaa kuzimia, wengine kujeruhiwa na kisha mabomu kadhaa ya machozi kuvurumishwa na polisi kutawanya maelfu ya wafuasi muda mfupi baada ya kumalizika.
Hali ya mkanganyiko katika mkutano huo wa Lowassa, anayeungwa pia na muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), ilianza kuonekana mapema wakati maelfu ya watu walipojitokeza kwenye viwanja vya Tangamano. Baadhi ya watu, hasa wanawake walijikuta wakiwa hoi hoi kutokana na joto na kukosa hewa, hali iliyowalazimu wahudumu wa Msalaba Mwekundu kuingilia kati na kutoa huduma ya kwanza kwani wengi wao walionekana wakizimia na kuanguka chini.
“Asanteni sana kwa mapokezi yenu. Hali iliyopo sasa sio nzuri…asanteni tena kwa mapokezi mazuri," alisema Lowassa kabla ya kuomba kura na kutaka mkutano huo usitishwe kwa kuhofia usalama wa watu kwenye uwanja huo ulioonekana kuwa mdogo.
“Katika hali hii, niseme tu nimefika kuwaombeni kura,” alisema Lowassa, kabla Meneja wa kampeni, John Mrema hajapanda jukwaani na kutangaza kuahirisha mkutano huo hadi siku nyingine kwa kuhofia kuwa msongamano huo ungeweza kusababisha vifo.
“Tunalazimika kuahirisha mkutano huu wa mgombea urais kwa hofu ya watu kufariki,” alisema Mrema na kuwaomba wananchi hao kuondoka.
Hata hivyo, umati wa watu uligomea tangazo hilo, ukimtaka Lowassa kuendelea kuzungumza nao.
Tangazo la kuahirishwa kwa mkutano huo lilikuja muda mfupi baada ya Lowassa kukaribishwa na Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ili azungumze na wananchi.
Hali hiyo iliufanya uongozi wa kampeni uliokuwapo kuamua kutengua uamuzi wao wa awali wa kusitisha mkutano huo na kumruhusu Lowassa kuzungumza na wananchi.
Aliposimama, Lowassa aliwasalimu kwa salamu ya People’s na wao wakajibu kwa sauti kubwa Power. Akizungumza na wananchi hao kwa mara ya pili, Lowassa alisema akichaguliwa atafufua Bandari ya Tanga, atafufua reli,
kufufua viwanda na kuboresha kilimo.
Hata hivyo, wananchi walisikika wakimtaka azungumzie suala la mwanamuziki Babu Seya, naye akasema akichaguliwa kuwa rais, atalishughulikia suala hilo kwa mujibu wa sheria.
Sumaye alipopata nafasi ya kuzungumza, aliwashukuru wana Tanga kwa kuhudhuria kwa wingi mkutano huo, huku akiwapa pole kwa msongamano mkubwa uliokuwepo.
Aliwaomba watu waliokuwa sehemu mbalimbali uwanjani hapo kukaa chini na wale ambao walikosa hewa wasaidiwe mara moja, hasa wanawake na watoto
MABOMU YARINDIMA
Baada ya mkutano kumalizika, baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo walijikuta wakivurumishiwa mabomu ya machozi na polisi baada ya kuonekana wakiandamana huku wengine wakikimbia mchakamchaka na kupita jirani na ofisi ya CCM katika Barabara ya 20 jijini hapa. Mtaani hapo, pia kuna ofisi ya CUF ambayo ina ngome yake ya kutumainiwa jijini hapa.
Makundi ya wananchi hao, hasa vijana walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifia Lowassa kuiponda CCM, hali iliyozua hofu kuwa pengine panaweza kuibuka mtafaruku kwa kufanya vurugu katika ofisi za CCM.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi jijini Tanga hakupatikana jana kuzungumzia hali hiyo kiundani.
LOWASSA ATAKA SIKU 100
Awali, akiwa katika Jimbo la Bumbuli, Lowassa alisema anahitaji siku 100 tu za kuwa Ikulu baada ya kuapishwa ili amalize kero kuhusia na ukosefu wa dawa hospitalini, madai ya walimu na pia kumaliza matatizo ya watumishi wote wa umma yanayohusiana na maslahi yao.
Alisema ana uhakika wa kushughulikia matatizo hayo ndani ya siku chache baada ya kushinda uchaguzi mkuu Oktoba 25 na kuapishwa kwa vile matatizo hayo anayajua vizuri na hivyo hakuna sababu ya kuchelewa katika kuyapatia ufumbuzi.
"Matatizo ya walimu na watumishi wengine nayajua... jitokezeni kwa wingi siku ya kupiga kura na kuleta mabadiliko," alisema.
Alisema kuweka dawa katika zahanati na hospitali hizo kutaenda sambamba na uwepo wa wataalamu mbalimbali.
Kadhalika, Lowassa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu katika awamu ya kwanza ya Rais Jakaya Kikwete, alisema matatizo ya ukosefu wa dawa katika zahanati, vituo vya vya na hospitali za umma yatafikia ukomo ndani ya siku hizo 100 atakazokuwa madarakani kwani eneo hilo ni miongoni mwa vipaumbele vyake vikubwa pindi akichaguliwa na kuwa rais wa awamu ya tano.
Pia, Lowassa aliahidi kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu baina ya wananchi wanaojihusisha na kilimo cha chai Bumbuli na wawekezaji, Kiwanda cha Chai cha Mponde kinachodaiwa kufungwa kwa sababu za kisiasa, akisema kuwa tatizo hilo litabaki kuwa historia ndani ya miezi sita ya kuwa kwake madarakani.
"Tumechoka... amekuja Mkuu wa Mkoa, amekuja Rais, amekuja Makamba, hakuna kilichofanyika.
Nawahakikishia nitamaliza tatizo hili," alisema Lowassa na kuongeza:
"Nitahakikisha tatizo hili linapata ufumbuzi, wakulima wanauza chai yao na kiwanda kinafanya kazi," alisema Lowassa na kuibua shangwe kubwa.
Katika hatua nyingine, Lowassa aliwataka wananchi wa Bumbuli kutofanya makosa kwa kumchagua tena mbunge anayetetea nafasi yake jimboni humo, January Makamba, kwa kudai kuwa yeye (Makamba) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawana tena uwezo wa kushughulikia kero zao.
Aliongeza kuwa mabadiliko ya kweli kwa Watanzania yatapatikana kwa kuiondoa CCM madarakani na hivyo akamshauri Makamba kuihama CCM na kutua Ukawa kwani yeye bado ni kijana na hivyo hana sababu kubaki katika chama ambacho mwisho wake wa kuongoza nchi utafikiwa baada ya uchaguzi Oktoba 25.
Lowassa aliendelea kuahidi kuanzisha benki maalumu kwa ajili ya mama lishe na waendesha bodaboda kuweza kupata mikopo mbalimbali kwa ajili ya kujikwamua na umaskini.
“Serikali yangu nitaiongoza kwa ‘speed’ 120, itakuwa ya vitendo zaidi badala ya longolongo, magoigoi wote watabaki CCM,” alisema.
Aidha, alirejelea kauli yake ya siku zote kuwa anauchukia umaskini na amechoshwa kusikia kero za michango ya shule, dawa na huduma duni za matibabu na kwamba ndani ya miaka mitano Tanzania itabadilika.
*Imeandikwa na John Ngunge na Dege Masoli, Tanga-NIPASHE