Mgombea urais wa UKAWA Mh Edward Lowassa ameingia kwa kishindo katika mkoa wa Kagera na amesema akichaguliwa kuwa rais mikoa yenye uhakika wa uzalishaji ukiwemo wa kilimo inapewa kipaumbele kinachostahili na wakulima wanapewa mikopo ya kuanzia miaka 5 hadi 15 na wanakuwa mfano wa kuigwa katika kupambana na umaskini.
Mh Lowassa ambaye amefanya mikutano katika majimbo ya Kerwa Karagwe, Mulaba kusini na kaskazini amesema hatua ya wananchi wa mikoa yenye fursa kubwa ya uzalishaji kama Kagera wanakabiliwa na umaskini ni dalili za kutosha kuonyesha kuwa lipo tatizo la mfumo wa utawala na ndio maana anaomba nafasi ya kuliondoa.
Aidha amesema sera za UKAWA zimeweka wazi jinsi itakavyoleta mapinduzi ya kiuchumi kupitia kilimo ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho makubwa kuanzia kwa maafisa ugani, ili wawawezeshe wakulima kulima kibiashara kuwa wa kwanza kuachana na umaskini.
Akifafanua baadhi ya sera zilizoko kwenye ilani ya UKAWA waziri mkuu awamu ya tatu Fredrick Sumaye amesema kupanda kwa gharama za maisha kushuka kwa uzalishaji ni miongoni mwa athari zinazo sababishwa na serikali ya CCM iliyojaa maneno bila vitendo na tatizo ambalo dawa yake iko mikononi mwa Lowassa.
Mh Lowassa anaendelea na kampeni zake katika jimbo la Bukoba mjini ambalo wananchi wameshaanza shamra shamra za maandalizi na mapokezi huku mji mzima ukiwa umejaa mabango na picha za Mh Lowassa na wagombea wa UKAWA.
Social Plugin