Tukio hilo limetokea Septemba 6, mwaka huu, baada ya watu hao kunywa juisi na kula chakula kilichoandaliwa katika sherehe hiyo.
Baada ya muda mfupi, waalikwa hao walianza kuumwa matumbo na kuharisha mfululizo hali iliyofanya kukimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Kelvini Chayonga, alisema tukio hilo lilitokea siku hiyo mchana.
Alisema wagonjwa wote walipelekwa kwenye zahanati ya kijiji hicho, lakini hali ilivyozidi kuwa mbaya walihamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa matibabu zaidi.
Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Letisia Philemon, alisema baada ya kula na kunywa juisi hiyo, walianza kuhisi maumivu makali.
“Tulikunywa vizuri ile juisi na chakula cha mchana, lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda, ndivyo maumivu yalivyokuwa yakizidi kunibana, hadi tukakimbizwa hospitali,” alisema.
Naye bwana harusi, Christian Lugonde alisema amesikitishwa mno na tukio hilo, kwani baada ya kuwa la furaha liligeuka kuwa huzuni.
Alisema juisi hiyo ilitengenezwa na mama yake wa kambo, ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwenye harusi hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo, Dk. Kizito Luhamvya, alisema walianza kupokea waathirika saa tano usiku na kufikia jana asubuhi walikuwa wamefikia 89.
Alisema baada ya kuwapima wote, 68 wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani, lakini 21 wanaendelea na matibabu zaidi.