Na Kadama Malunde-Shinyanga
Serikali imesema imejipanga vyema kukabiliana na watu waliojiandaa kufanya vurugu ikiwemo kuzuia wanawake na wazee wasipige kura siku ya uchaguzi mkuu nchini utakaofanyika Oktoba 25,2015.
Hayo yamesemwa juzi na mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro(pichani) wakati akizungumza na wanawake wa manispaa ya Shinyanga katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa NSSF mjini Shinyanga uliolenga kujadili mambo mbali mbali ya kimaendeleo ikiwemo ulinzi na usalama kwa wanawake siku ua uchaguzi.
Matiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama katika wilaya ya Shinyanga alisema serikali haiko tayari kuona amani ya nchi inachezewa na watu wachache hivyo serikali itahakikisha kuwa amani ya nchi inalindwa muda wote.
"Acheni kusikiliza maneno ya majukwaani,kuna watu wanawatisha kuwa siku ya uchaguzi watawazuia wanawake na wazee wasipige kura,hii haikubaliki,asiwatishe mtu,kila mwananchi ana haki ya kupiga kura ili kupata kiongozi anayemtaka,hivyo jitokezeni kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi",alisema Matiro.
"Wanaotishia kufanya fujo siku ya uchaguzi, tutakula nao sahani moja,tunataka utunza amani ya nchi,hakuna wa kuwatisha,tutaweka ulinzi wa kutosha,wala msiogope ,wanawake ni jeshi kubwa,jitokezeni kwa wingi kuchagua viongozi mnaowataka",aliongeza Matiro.
Katika hatua nyingine aliwataka wananchi kutunza kadi zao za kupigia kura na kutouza kadi hizo kwani kufanya hivyo ni kupoteza haki yao ya kupiga kura.
Mkuu huyo wa wilaya alitumia fursa hiyo kuwataka wanawake kujishughulisha na shughuli mbalimbali za maendeleo kwa kujiunga na vikundi vya wajasiriamali ili serikali iweze kuwasaidia kwa urahisi badala ya kufuata mtu mmoja mmoja.
Alisema ni aibu kubwa kwa karne hii wanawake kuendelea kuwa tegemezi kwa wanaume hivyo kuwataka wajishughulishe katika shughuli za maendeleo ili kupiga vita umasikini katika jamii.
Social Plugin