Ombi la Chadema la kutaka wataalamu wa Tehama wa vyama vya siasa na waangalizi wa kimataifa waruhusiwe kukagua programu itakayotumika kuhesabu kura za urais, limesababisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kukitaja chama hicho kuwa ndicho pekee kinachoipa shida katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva ambaye hata hivyo alisema Tume yake itakutana na wawakilishi wa vyama vyote muda mfupi kabla ya siku ya upigaji kura ili watoe madukuduku waliyonayo.
“Tunasubiri walete hilo ombi. Lakini hata wasipofanya hivyo tutakuwa na kikao na vyama vyote vya siasa baada ya kumalizana na wadau wengine. “Chadema wana wasiwasi mwingi na ndicho chama kinachotupa shida mara nyingi.
Tukifanya hivi, wao wanataka hivi,” alisema Jaji Lubuva alipokuwa akijibu maombi ya Chadema yaliyotolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wake, John Mnyika alipozungumza na vyombo vya habari.
Mnyika aliitaka NEC kuruhusu wataalamu wa Tehama wa vyama vya siasa na waangalizi wa kimataifa nao waende NEC na wataalamu wao kuhakiki mfumo utakaotumika kupokelea kura za urais kwa lengo la kujua kama uko salama ili kuzuia uchakachuaji wa matokeo.
Mnyika alidai kuwa kuna mazingira ya kupigwa ‘bao la mkono’ yanayotengenezwa na ndiyo maana ni muhimu mambo yote yakawekwa wazi ili kuzuia uchakachuaji wa matokeo. “Lubuva akubali kuanzia sasa tuchambue huo mfumo na wataalamu wetu waukague ili wajue kama uko salama usije ukawa ni wa kuiba kura na kutupiga ‘bao la mkono’,” alisema Mnyika.
Mbali na hilo, Mnyika alidai kuwa anashangaa kwa nini NEC hadi sasa haijawasilisha daftari la awali la wapigakura kwa vyama vya siasa ili walihakiki. “Kwa nini hadi sasa hawajatukabidhi daftari, lazima tupewe kama ilivyofanyika mwaka 2010,” alisema Mnyika na kuongeza: “Suala la kwamba NEC inasema uhakiki umefungwa wakati sisi hatujakabidhiwa hilo daftari kulihakiki, kuna mazingira ya bao la mapema la mkono.”Mnyika alisema mwaka 2010, daftari hilo lilivisaidia vyama vya siasa kuwaonyesha wananchi ambao walikosa majina yao vituoni kuwaelekeza vituo vyao kutokana na majina kuwapo kwenye daftari lakini yakikosekana kwenye orodha zinazobandikwa vituoni. “Daftari hili ni muhimu sana, mwaka 2010 tuliweka dawati letu kwenye vituo.
Wananchi ambao walifika kituoni na kukosa majina yao kwenye orodha iliyobandikwa tuliwaambia waende kwenye dawati la Chadema waangaliziwe kwenye daftari na walipokuta majina yapo tuliwaambia wapige kura na walifanya hivyo bila matatizo,” alisema Mnyika. Aliwataka wananchi kuwa makini na suala hilo na kuhakikisha wanapiga na kulinda kura ili kuzuia uchakachuaji wa matokeo.
Pamoja na kwamba Jaji Lubuva alisema matokeo yote yatabandikwa vituoni, hivyo wananchi wapige kura na kuondoka, Mnyika alipinga na kuwataka wananchi kutomsikiliza kwani kuondoka vituoni kunatoa mazingira ya kuibwa kura.
Hata hivyo, Mnyika alisema pamoja na mazingira mbalimbali ya bao la mkono yanayotengenezwa, mwaka huu ni wa mabadiliko, hivyo wana Ukawa wasikate tamaa.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin