Mke wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mama Salma Kikwete,ameitaka jamii ya wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara kwa ujumla,kuacha mara moja tabia ya kuwakandamiza ikiwemo ya kutumikisha watoto wa kike,hatua ambayo amesema imekuwa ikichangia kudhorotesha kwa kiasi kikubwa maendeleo ya wanawake wa mkoa wa Mara.
Mama Salma Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa taasisi ya wanawake na maendeleo wama,ametoa kauli hiyo wilayani Tarime baada ya kuzindua shule mpya ya sekondari ya Julius Kambarage Nyerere katika kijiji cha Nyamwaga, ambayo imejengwa kwa shilingi bilioni 1.7 chini ya ufadhili wa kampuni ya ACACIA Mining kupitia mgodi wake wa mgodi wa North Mara wilayani Tarime.
Kwa upande wake kaimu meneja mkuu wa mgodi wa North Mara Bw.Jimmy Ijumba,amesema mradi huo wa ujenzi wa shule hiyo mpya ya sekondari,ni sehemu ya miradi mingi ya kijamii inayotekelezwa na mgodi wake katika vijiji zaidi ya kumi vinavyozunguka eneo la mgodi huo.
Naye afisa mtendaji wa kijiji hicho cha Nyamwaga Bw.James Wambura,pamoja na kupongeza mafanikio hayo makubwa,lakini amesema changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo ni pamoja na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Chanzo-ITV
Social Plugin