Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGOMBEA UBUNGE ATEKWA HUKO SIMIYU…HAJULIKANI ALIPO MPAKA SASA….

 
Jeshi la Polisi mkoani Simiyu limethibitisha kutekwa kwa mgombea ubunge Jimbo la Bariadi, kupitia chama cha ACT Wazalendo Masunga Ng’hozo na watu wasiojulikana.


Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Gemini Mushy amesema kuwa tangu kutoweka kwa mgombea huyo, simu yake imekuwa ikitumika kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa wazazi wake.

Amesema kuwa ujumbe huo umekuwa ukiwataka wazazi wake kutoa kiasi cha fedha shilingi milioni mbili na nusu ndipo waweze kumwachia huru vinginevyo wajiandae kupokea maiti ya mwili wa mtoto wao.

Kamanda Mushy ameeleza kuwa mgombea ubunge huyo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, (SAUT) kampasi ya Mbeya alitoweka Septemba 27 mchana akitokea ofisi ya chama hicho mkoa.

Amesema kuwa jeshi la polisi liliweza kupata taarifa rasmi ya kutekwa mgombea huyo tarehe 29 Septemba mwaka huu, ambapo ameeleza kuwa mpaka sasa siku ya nne hajulikani alipo na yuko katika mazingira ya usalama kiasi gani.

“ Ni kweli tumepata taarifa za mgombea ubunge huyo kutekwa na mpaka sasa ni siku ya nne hatujafahamu yuko sehemu gani na katika mazingira gani lakini jeshi la polisi kwa kushirikiana na wazazi wake na watu wake wa karibu tunaendelea kufanya uchunguzi ili tubaini mahali alipo na wahusika wa tukio hilo” amesema Kamanda Mushy.

Aidha Kamanda Mushy amesema kuwa kabla ya mgombea huyo kutekwa aliondoka katika ofisi ya chama hicho Mkoa, alikiwa amebeba begi lake huku akiwa anaongea na simu huku akimtaka dereva wa gari lake pamoja na fundi mitambo kumsubiri ofisini hapo.

Kufuatia tukio hilo Kamanda Mushy ameeleza kuwa jeshi lake linaendelea kufanya uchunguzi kwa njia ya mitandao ili kubaini ujumbe wa vitisho unatokea maeneo gani ikiwa pamoja na kuwakamata wahusika wanaoendelea kutumia simu ya mgombea huyo.

Kwa upande wake Katibu wa ACT-Wazalendo, Simiyu, Matondo Maduhu amesikitishwa na kulaani kitendo hicho, hivyo wanaliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi mapema ili kubaini mahali na kunusuru maisha ya mgombea huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com