Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAARIFA YA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA SHINYANGA SIKU YA WADAU WA HABARI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU TANZANIA




Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga,ndugu Kadama Malunde akitoa taarifa ya klabu ya waandishi wa habari mkoa huo juzi Oktoba 02,2015 katika ukumbi wa Katemi Hotel mjini Shinyanga.Mkutano huo ulikutanisha wadau mbalimbali wa habari mkoani Shinyanga,ambao kwa pamoja walijadili namna ya kushirikiana ili kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unakuwa huru na wa haki-Picha na John Mponeja-Malunde1 blog



TAARIFA YA KLABU YA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA SHINYANGA SIKU YA WADAU WA HABARI

Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club- SPC) ilipata usajili wa kudumu mwaka 2003 kufuatia mkutano mkuu uliofanyika mjini Shinyanga na kuwakutanisha waandishi wa habari 13 waanzilishi wa klabu.

Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga ni mwanachama wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini Tanzania( Union of Tanzania Press Clubs-UTPC) pia inaitambua kama asasi mwamvuli na inafuata masharti yote ya UTPC na ndiyo iliyotoa agizo la kufanyika kwa mikutano ya wadau wa habari kote nchini,mikutano yote ina kauli mbiu “Uchaguzi Huru na Haki,bila waandishi wa habari kuzingatia maadili ni ndoto”.

Miongoni mwa malengo ya Klabu ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga ni Kulinda wanachama wake dhidi ya vizuizi vinavyowakabili ambavyo vinasababisha kutokeleza majukumu yao ya uandishi wa habari.

Lengo jingine ni kuwezesha ushirikiano miongoni mwa waandishi wa habari, vyanzo vya habari na wadau mbalimbali wa habari kama mliomo kwenye ukumbi huu.

Klabu hii pia ina lengo la kuboresha kiwango cha ukusanyaji na upashanaji habari na Kuinua viwango vya taaluma katika tasnia ya uandishi wa habari nchini.

Hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kuwa na jumla ya wanachama 38 kutoka wanachama 13 waanzilishi wa Klabu hii.

Kati ya wanachama hawa 38 ,18 wanatoka wilaya ya Shinyanga,19 wilaya ya Kahama na mmoja kutoka wilaya ya Kishapu lakini pia kati yao wanawake ni 15 na wanaume ni 23 na wote wanafanya kazi katika Magazeti, Radio, Televisheni na Mitandao mbalimbali ya kijamii zikiwemo Blogu.

Ni ukweli usiopingika kuwa Waandishi wa habari mkoani Shinyanga wamekuwa mstari wa mbele katika kuipasha habari jamii kuhusu matukio yanayoendelea, kuielimisha juu ya masuala mbalimbali, kukosoa, kuhamasisha shughuli za maendeleo na mengine mengi.

Hakuna asiyetambua kazi kubwa iliyofanywa na waandishi wa habari katika kuutangaza mkoa wa Shinyanga juu ya shughuli za maendeleo mkoani hapa.

Waandishi wa habari mkoani Shinyanga ndiyo waliofanikisha hata waathirika wa mvua ya upepo mkali na mawe katika kata ya Mwakata wilayani Kahama kupata misaada ya hali na mali kutoka kwa wadau mbalimbali nchini Tanzania.

Lakini pia ni waandishi wa habari wa mkoa wa Shinyanga kupitia kalamu zao ambao wamekuwa wakitoa elimu kuhusu madhara ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) na vikongwe kwa imani za kishirikina,matukio ambayo katika mkoa wetu yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Sote tunatambua kuwa nchi yetu pendwa ya Tanzania mwezi huu wa kumi yaani Oktoba 25 kutafanyika uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,wabunge na madiwani.

Kutokana na uzito wa tukio hilo, waandishi wa habari mkoani hapa wamepatiwa mafunzo mbalimbali kuhusu namna ya kuandika na kuripoti habari za uchaguzi ambapo walikumbushwa pia juu ya kuzingatia maadili yao ya kazi ili kuepuka kuiingiza nchi katika machafuko kwani tumeshuhudia amani ya nchi nyingi ikitoweka kutokana na waandishi wa habari kwenda kinyume na maadili yao.

Mafunzo hayo yaliyolenga kuwakumbusha na kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuhusu uandishi wa habari za uchaguzi yametolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na Taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayohusika na vyombo vya habari BBC Media Action.

Katika tukio hili muhimu la kitaifa, Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga inawasisitiza waandishi wa habari kuandika habari za uchaguzi kwa kuzingatia maadili ya kazi yao.

Ili kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unakuwa huru na haki ,Klabu ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga inawataka waandishi wa habari kuzingatia maadili yao ikiwemo kuepuka rushwa,kuandika habari za Ukweli na uhakika ikiwa ni pamoja na kuhakiki taarifa kabla ya kuitangaza au kuichapisha.

Waandishi wa habari pia wanatakiwa kuripoti habari kwa usawa kwa wagombea na vyama vyote vya siasa yaani Kutoegemea upande wowote kwa kupendelea mgombea au chama fulani cha siasa.

Aidha Maadili ya waandishi wa habari yanawataka kutojiingiza kwenye siasa ikiwemo kushabikia mgombea ama chama chochote cha siasa kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki wagombea na vyama vingine vya siasa ,matokeo yake kuibuka kwa malalamiko kutoka upande mwingine.

Pia ili kuliepusha taifa lisiingie katika machafuko katika kipindi hiki cha uchaguzi waandishi wa habari wanatakiwa kuepuka kuandika,kutangaza ama kuchapisha habari zinazoibua chuki *Hate Speech* kwa mtu binafsi,kundi la watu ama chama fulani cha siasa.

Tunaamini kabisa kuwa, uchaguzi mkuu utakuwa huru na haki endapo pia waandishi wa habari watapata ushirikiano kutoka kwa wadau wote mfano pale wanapohitaji taarifa mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya uandishi,ambapo tunawaomba pia watendaji wenye tabia ya kuficha taarifa kuachana na tabia hizo.

Kama kauli mbiu ya mkutano huu inavyosema, “Uchaguzi Huru na Haki,bila waandishi wa habari kuzingatia maadili ni ndoto”,Tunasisitiza zaidi waandishi wote wa habari kuandika,kuchapisha, kuripoti na kutangaza habari za uchaguzi kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.

Tanzania ni yetu,tuepuke vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa wakati huu muhimu ambapo wananchi wanakwenda kuchagua viongozi watakaolingoza taifa hili kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Tukumbuke “Kuna maisha baada ya Uchaguzi”.

Asanteni kwa kunisikiliza..

Imetolewa na Kadama Malunde

Mwenyekiti SPC

02.10.2015



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com