Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe(aliyesimama pichani) amewataka wananchi mkoani Shinyanga kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa kipindupindu ambao tayari umeibuka mkoani Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Shinyanga Dkt Kapologwe amesema tayari watu 12 wamelazwa katika kambi maalum iliyotengwa jirani na hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
Amesema kati ya wagonjwa 12 waliolazwa 8 wamebainika kuwa na vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu hivyo kuwataka wakazi wa Shinyanga kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo.
"Ni kweli Mkoa wa Shinyanga umekumbwa na kipindupindu....Kati ya wagonjwa 12,tuliowapokea watatu wanatoka Kitangiri Shinyanga, wawili wanatokea Majengo Mapya,watatu kutoka Mwawaza katika manispaa ya Shinyanga na wanne wanatoka wilayani Kishapu,tayari tumeshaweka kambi maalumu kwa ajili ya kulaza wagonjwa wa kipindupindu,madaktari wamejiandaa na dawa muhimu zipo hivyo tunawashauri wananchi pindi tu waonapo dalili za ugonjwa huu kama vile kuumwa tumbo ghafla wawahi hospitali",amesema Dkt Kapologwe.
"Kipindupindu kinatokana na kula kinyesi kilichochanganikana na maji,chakula ama kitu chochote...tunaomba wananchi waepuke mikusanyiko ya watu wakati wa ulaji vyakula,wananchi wale vyakula vya moto,pia waepuke kula bila kunawa..kubwa zaidi tunataka wananchi waimarishe usafi katika maeneo yao",ameongeza Dkt Kapologwe.
Hata hivyo amesema wamepiga marufuku harusi kwani zinahusisha ulaji vyakula hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kuenea kwa ugonjwa huo.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog