Kufuatia madhara yaliyotokea katika mgodi wa dhahabu wa Nyangalata na kusababisha waokoaji kushindwa kuwaokoa watu sita ambao walikaa chini ya mgodi kwa siku arobaini na moja kutokana na kukosa vifaa vya uokoaji baraza la taifa la uhifadhi wa mazingira NEMC limeifunga migodi mitatu ya dhahabu iliyoko katika kijiji cha Bugarana wilayani Kahama mkoani Shinyanga ili kuepusha madhara kama hayo yasitokee katika migodi mingine.
Akizungumza wakati wa kufunga migodi hiyo ambayo ni Tanzania Vestness International Mining, Nitaka Mining na Batalion Mining iliyoko wilayani Kahama Shinyanga afisa mwandamizi wa mazingira NEMC Dr.Mandoshi Makene amesema hali ya uharibifu wa mazingira katika maeneo ya migodi nchini imekuwa ikiongezeka na kutishia maisha ya watanzania hivyo amewataka wawekezaji na wachimbaji kufuata sheria na maelekezo yanayotolewa na NEMC vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
Naye mwanasheria wa NEMC Bw.Manchare Heche Suguta ameeleza hatua zinazochukuliwa kwa wawekezaji wanaobainika kukiuka sheria na taratibu za utunzaji wa mazingira huku mmiliki wa mgodi wa madini wa Tanzania Vestness International Mining ambaye ni mchina akishangaza kwa kutoelewa kuongea kingereza wala kiswahili mbali na kuishi nchini kwa siku nyingi hali iliyosababisha zoezi kuchukua muda mrefu kwakuwa hakuna mkalimani wa kutafsiri lugha ya kichina.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyakazi wa migodi iliyofungwa wamelalamika hatima ya mishahara yao na kudai hawajalipwa kwa zaidi ya miezi mitatu huku baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na migodi hiyo wakiziomba mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali vya uchimbaji kushirikiana na nemc ili kulinusuru taifa na janga la mabadiliko ya tabia nchi.
Via>>>ITV
Social Plugin