Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo kabla ya kufikwa na umauti
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo enzi za uhai wake
Mji wa Geita umezizima kwa simazi,vilio na majonzi baada ya kutokea kifo cha kinyama cha aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Busanda kupitia Chadema na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia Maendeleo Chadema mkoa wa Geita,Alphonce Mawazo.Anaripoti mwandishi wa Malunde1 blog mkoani Geita,Victor Bariety.
Tukio hilo limetokea majira ya saa tano asubuhi katika Kijiji cha Katoro kata ya Ludete wilayani Geita baada ya Mawazo kuvamiwa na watu wasiojulikana ambao walimshambulia kwa silaha zinazodaiwa kuwa ni marungu,mapanga na mashoka na kumkata shoka katikati ya kichwa.
Kiongozi huyo kabla ya kukumbwa na mkasa huo alikuwa Katoro kwenye Kikao cha ndani kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Ludete ambao unatarajiwa kufanyika Kesho,Novemba 15,2015 baada ya kutofanyika Oktoba 25 mwaka huu kutokana na vifaa vya kupigia kura zikiwemo karatasi kutofika kwenye kata hiyo.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Geita,Dk.Adamu Sijaona ameiambia Malunde1 blog kuwa ,walimpokea majeruhi saa 9 alasiri akiwa katika hali mbaya ambapo alikuwa hajitambui.
“Alikuwa na majeraha makubwa kichwani,katikati ya kichwa..alikuwa amepoteza fahamu kabisa,na walikuwa wamemchalewesha amefariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hapa kutokana na kuvuja damu nyingi,wakati madaktari wakijaribu kuokoa maisha yake”,amesema Sijaona.
Amesema mwili wa Kiongozi huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Geita wakati taratibu zingine zikiendelea.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakutaka kutajwa majina yao wamesema baada ya watu hao kumshambulia kwa mapanga,shoka na marungu walimtelekeza Mawazo barabarani na kutokomea kusikojulikana.
Inaelezwa kuwa baada ya tukio hilo wanachama wa Chadema waliokuwa eneo la Kikao walipata taarifa za tukio hilo na kwenda kumchukua eneo alilokuwa amedondoka na kumkimbiza katika Kituo cha Afya cha Katoro na baadaye hospitali ya wilaya ya Geita.
Taarifa za awali zinadai kuwa,Chadema chini ya Mwenyekiti huyo walikuwa na mkutano wa ndani kwenye ukumbi wa Makungu Uliopo Mtaa wa CCM mjini Katoro na akatokea kijana mmoja nje ya ambaye walimshukia kuwa anarekodi mkutano wao.
“Baadaye vijana wa Chadema walitoka nje na kumnyang’anya simu yake ..ndipo zikatokea vurugu..lakini wakati huo Mawazo alikuwa ameshatoka,ndipo tukapata taarifa za kifo cha Mawazo kufika pale tulikuta amefariki”,amesema mmoja wa wanachama wa Chadema.
Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Latson Mponjoli alipopigiwa simu ili kutoa ufafanuzi wa tukio hilo alisema’’ Nipo nje ya ofisi na mimi ndiyo nafuatilia ili nipate data za kutosha kuhusiana na tukio hilo,na siwezi kukueleza ni muda gani nitakuwa tayari,naomba uniache kwanza’’alisema Mponjoli na kukata simu.
Na Victor Bariety- Malunde1 blog Geita