Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) wilaya ya Shinyanga mjini Samson Ng'wagi akitoa tamko la vijana katika ofisi za Chadema wilaya kwa waandishi wa habari juu ya mwenendo mzima wa uchaguzi na matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi-Picha na Kadama Malunde
Kulia ni Katibu wa BAVICHA wilaya ya Shinyanga mjini Zainab Heri
Kushoto ni mjumbe wa BAVICHA wilaya ya Shinyanga mjini Christopher Machiya
Katibu wa BAVICHA wilaya ya Shinyanga mjini Zainab Heri akizungumza katika ofisi za Chadema wilaya ya Shinyanga mjini leo
Baraza la Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) wilaya ya Shinyanga mjini wamewataka wabunge wa UKAWA waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita kupigania kupatikana kwa katiba mpya itakayowezesha kupatikana kwa tume huru ya taifa ya uchaguzi ili kuepusha vitendo vya kubakwa kwa demokrasia nchini.
Rai hiyo imetolewa LEO na mwenyekiti wa Bavicha wilaya hiyo Samson Ng’wagi wakati akitoa tamko la vijana kwa waandishi wa habari juu ya mwenendo mzima wa uchaguzi na matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.
Ng’wagi aliwataka wabunge wa ukawa waliopata nafasi ya ubunge kusimamia upatikanaji wa katiba mpya hali itakayosaidia kuwa na tume huru ya uchaguzi na kuondoa hali ya sintofahamu katika chaguzi zingine zijazo.
Alisema pamoja na kwamba uchaguzi umekwisha na matokeo kutangazwa wao kama vijana hawakuridhishwa na mwenendo mzima wa uchaguzi kutokana na hujuma na vitendo vya rushwa kutawala huku vyombo vya dola vikitumika kukisaidia chama tawala ili kiendelee kubaki madarakani .
“Hatukuwa na demokrasia wakati wa uchaguzi,tuliona utulivu tu wananchi,sisi vijana wa wilaya hii tumeshuhudia vitendo vingi vya hujuma vilivyofanywa na vyombo vya dola ikiwemo vijana wengi kukamatwa na polisi kwa sababu zisizoeleweka,vitendo vya rushwa vilitawala lakini wahusika hawakuchuliwa hatua licha ya kuwepo kwa ushahidi kuwa wanatoa rushwa”,alieleza Ng’wagi.
“Tumeshuhudia demokrasia ikibakwa,naomba wabunge waliopata nafasi ya kuingia bungeni kupigania maslahi ya wananchi na kuhakikisha katiba mpya inapatikana hali ikayosababisha kukuza kiwango cha demokrasia nchini Tanzania”,aliongeza Ng’wagi.
Naye Katibu wa BAVICHA wilaya ya Shinyanga mjini Zainab Heri alisema ni vyema tume ya uchaguzi Zanzibar ikamtangaza Maalim Seif kuwa ndiye mshindi aliyechaguliwa na wananchi kuliko kufanya vitendo vinavyoashiria kubaka demokrasia hali ambayo inaweza kusababisha wananchi kukosa imani na serikali itakayoingia madarakani.
Nao baadhi ya wanachama wa Chadema walidai kuwa mwenendo mzima wa uchaguzi mkuu 2015 uligubikwa na vitisho kutika vyombo vya dola ikiwemo jeshi la polisi na kusababisha asilimia kubwa ya watanzania kuogopa kujitokeza kupiga kura.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog