Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JINSI CHADEMA WALIVYOIBWAGA SERIKALI KESI YA KIGOGO WA CHADEMA ALIYEUAWA HUKO GEITA

 
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza, imetupa zuio la Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, RPC Charles Mkumbo kuzuia kuagwa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), marehemu Alphonce Mawazo.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Lameck Mlacha na kuwapa ruksa ndugu na viongozi wa chama hicho kutoa heshima za mwisho sehemu yoyote itakayofaa, huku akisema amri ya kamanda huyo wa Mwanza ni batili kisheria.

Katika hukumu hiyo, mahakama ilisema kuwa RPC Mkumbo amefanya kosa kubwa la kuvunja Katiba ya nchi, uhuru wa kuabudu na haki za binadamu kutokana na amri yake, huku akiwataka makamanda wengine nchini kutofanya makosa ya namna hiyo wakati wakitekeleza wajibu wao.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Mchungaji Charles Lugiko ambaye ni baba mdogo wa marehemu Mawazo, akiitaka mahakama hiyo kuondoa zuio la Kamanda Mkumbo la kutokuaga mwili huo Mwanza kwa kile alichodai kuna ugonjwa wa kipindupindu.

Pia Kamanda Mkumbo alisema taarifa za kiintelijensia zinaonyesha kuwapo uvunjifu wa amani wakati wa shughuli hiyo.

Katika kesi hiyo iliyosikilizwa na Jaji Mlacha kwa siku nne mfululizo, Kamanda Mkumbo aliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Seth Mkemwa na Emilly Kilia, huku John Mallya, James Milya na Paul Kipeja ambao ni wanasheria wa Chadema wakimtetea Lugiko.



HUKUMU YA JAJI MLACHA

Katika hukumu hiyo iliyochukua dakika 30, Jaji Mlacha alianza kusoma hoja zilizowasilishwa na pande zote na baadaye kuainisha makosa yaliyofanywa na Kamanda Mkumbo kwa kuzingatia jinsi alivyovunja Katiba ya Tanzania.

“Baada ya kuelezea hoja za pande mbili na kupitia vielelezo vilivyowasilishwa, mahakama yangu imebaini kuna tofauti kati ya tamko kimaandishi lililowasilishwa kwangu na video aliyokuwa akizungumza na waandishi, hii inaonyesha jinsi ilivyokuwa na upungufu, Mahakama Kuu ina uwezo wa kubatilisha amri yoyote iliyotolewa kama imetolewa kinyume na sheria na taratibu.

“Katika kesi, mahakama imeona kuna uhuru wa kuabudu ulizuiwa pasipo na sababu, sheria na Katiba ya nchi vimekiukwa na haki za binadamu zimevunjwa, ndugu wa marehemu ambaye ni mdai pamoja na marafiki, viongozi, wananchi pamoja na ndugu walikuwa na haki ya kumuaga marehemu Mawazo wakati na sehemu yoyote.

“Kazi ya dola ilikuwa ni kuandaa mazingira ya usalama ili shughuli za kuaga zifanikiwe, kigezo cha Kamanda Mkumbo kudai kulikuwa na intelijensia ya uvunjifu wa amani, alitakiwa kuwasiliana na ndugu wa marehemu pamoja na viongozi wa Chadema ili kuona namna ya kuepusha na kuimarisha usalama,” alisema.

Jaji Mlacha aliendelea kusema katika historia ya Tanzania kuna misiba mingi ya watu mashuhuri, viongozi na watu wa kawaida wamekuwa wakiagwa mkoa mwingine na kuzikwa sehemu nyingine, hivyo marehemu Mawazo kama alivyokuwa kiongozi, anapaswa kuagwa Mwanza kwa kuwa ndipo palipo na familia yake, viongozi wa kisiasa, wafuasi, isitoshe ndipo alipolelewa na baba yake mdogo hadi anakutwa na mauti.

Alisema suala la mawakili wa Kamanda Mkumbo kutumia historia ya marehemu Mawazo kujitetea mahakamani hakina umuhimu sana, hivyo mtu anapofariki ni vema mila, desturi na tamaduni zikazingatiwa, hivyo kama mahakama haiwezi kupuuza haki za msingi za mdai.

Jaji Mlacha alisema polisi wanapaswa kuzingatia sheria, Katiba na uhuru wa kuabudu wakati wakitekeleza wajibu wao huku akisisitiza hukumu hiyo kuwa fundisho kwa wengine wanaovunja sheria na haki za binadamu.

“Ni jambo la kusikitisha kuona polisi wakitumia nguvu kubwa kwenda kuwatawanya waombolezaji nyumbani kwa baba mdogo wa marehemu, isitoshe nyumbani kwa marehemu kuliwekwa ulinzi mkali, kilichotakiwa kufanywa na Kamanda Mkumbo, kabla ya kutoa amri ya kutoaga hapa Mwanza, alitakiwa awaite ndugu na kuwaeleza alichokusudia kukifanya ili kila mmoja atafakari athari zitakazotokea.



SHANGWE MAHAKAMANI

Shangwe na vigelele vililipuka mahakamani baada ya Jaji Mlacha kutoa hukumu hiyo, huku wananchi wakimbeba juu juu mwanasheria John Mallya aliyekuwa akiongoza jopo la wanasheria katika kesi hiyo.
Na Benjamin Masese-Mtanzania 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com